Kalemani akutana kwa dharura na bodi ya Tanesco

Waziri wa Nishati, Dk Medard Kalemani

Muktasari:

Kutokana na umeme kukatika mara kwa mara Waziri wa Nishati, Medard Kalemani amekutana kwa dharura na bodi ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco)

Dodoma. Waziri wa Nishati, Dk Medard Kalemani amekutana kwa dharura na bodi ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kutokana na tatizo la kukatika mara kwa mara kwa nishati hiyo.

Kukatika kwa umeme kumetajwa kusababishwa na kutoka kwenye Gridi ya Taifa

Akizungumza jana jioni Jumamosi Desemba 12, 2018 Kalemani amesema katika kipindi cha miezi miwili Gridi ya Taifa imetoka mara nne kuanzia Novemba 28 hadi Desemba 14, 2018.

Amesema kitendo hicho ni hatari kwa usalama wa Taifa ikizingatiwa kuwa nchi ina ziada ya umeme wa wastani wa megawati 252
Amesema nchi inapokuwa gizani hata kwa sekunde moja maana yake hakuna usalama na kutoa maelekezo kwa bodi hiyo kuchukua hatua.

“Lazima kuchukua hatua kuhakikisha hilo halijitokezi. Mwenyekiti (wa bodi) unda timu mahsusi kuanzia leo ya kuchunguza na kufuatilia jambo hilo kwa kushirikisha tasnia na taasisi mbalimbali si Tanesco pekee,” amesema.

“Ndani ya siku saba nipate matokeo ya nini chanzo cha tatizo hilo ili lisijirudie kabisa. Jambo hili linapotokea ina maana kuna uzembe katika usimamizi ama  kutofuatilia a maagizo ya Serikali.”

Amesema huenda jambo hilo huenda ni hujuma za baadhi ya watumishi waliokosa uzalendo na kuagiza bodi ichukue hatua kwa naibu mkurugenzi wa usambazaji na wa uzalishaji.