Kamishna aeleza alivyofuta umiliki

Dar es Salaam. Kamishna wa Ardhi Msaidizi Kanda ya Dar es Salaam, Mathew Nhonge (46) ameieleza Mahakama ya Wilaya ya Ilala kuwa hati 57 za viwanja vya mfanyabiashara Mohammed Kiluwa ziliondolewa umiliki katika daftari la usajili baada ya mshtakiwa kudaiwa kutoa rushwa kwa waziri.

Nhonge ambaye ni shahidi wa nne katika kesi ya kutoa rushwa kwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Wiliam Lukuvi, inayomkabili Kiluwa aliieleza jana mahakama hiyo alipokuwa akitoa ushahidi.

Kiluwa anayetetewa na Wakili Omar Madega, anakabiliwa na shtaka la kutoa rushwa ya Dola40,000 za Marekani.

Akiongozwa na wakili kutoka Takukuru, Maghela Ndimbo akisaidiana na Nikson Shayo, mbele ya Hakimu Mkazi Samuel Obasi, alidai chini ya kifungu cha 178 cha Sheria ya Ardhi namba 4, kamishna wa ardhi anaweza kuziondolea umiliki hati husika katika daftari la usajili kama mmiliki wake atabainika kujihusisha na vitendo vya rushwa.

Alieleza kuwa mshtakiwa aliomba kupimiwa viwanja 73 na Juni na Julai, mwaka huu alikuwa amepatiwa hati za viwanja 57, huku vikibaki 16 vilivyokuwa havijapatiwa hati.

Alidai kabla ya kumpatia hati hizo 57, Lukuvi alitoa masharti kwa mshtakiwa kuwa viwanja hivyo viendelezwe ndani ya miaka miwili na asipofanya hivyo atanyang’anywa kwa mujibu wa sheria.

“Julai 13, 2018 nilipigiwa simu na Waziri Lukuvi akinitaka nimfahamishe Kiluwa Julai 16 afike ofisini kwa waziri akiwa na hati hizo, nilifanya hivyo,” alidai Nhonge. Hata hivyo, wakili wa utetezi, Madega, alimhoji shahidi kwa nini walichukua uamuzi wa kuziondolea umiliki hati hizo wakati mshtakiwa bado hajapatikana na hatia.

Shahidi: Tulichukua uamuzi wa haraka kama sheria inavyosema, ni uamuzi wa kitaalamu na hayo yalifanyika chini ya kifungu 178 cha Sheria ya Ardhi namba 4 inayosema kamishna wa ardhi anao uwezo wa kuziondoa hati hizo katika daftari la usajili kama mhusika atabainika kujihusisha na vitendo vya rushwa.

Wakili Madega: Mahakama ikithibitisha Kiluwa hana hatia, je atarudishiwa hati zake?

Shahidi: Hakuna chochote kinachoweza kupinga uamuzi wa mahakama juu ya hati hizo.

Wakati huohuo, shahidi wa tano Colman Lubisa (36), ambaye ni mchunguzi kutoka Takukuru alidai baada ya kuweka kifaa cha kunasa sauti katika ofisi ya Waziri Lukuvi alisimama katika korido karibu na mapokezi ili aweze kuona mtu anayeingia kwa waziri.

Alidai mtuhumiwa alifika mchana na kuingia lakini baada muda mfupi aliingia Kassim Ephraim na kisha kumuita.

Baada ya kumaliza kutoa ushahidi, Hakimu Obasi aliahirisha kesi hiyo hadi leo itakapoendelea. Tayari mashahidi wanne wa upande wa mashtaka wamekwishatoa ushahidi wao dhidi ya Kiluwa akiwemo Waziri Lukuvi.