Kampuni saba za Uturuki zajipanga kuwekeza Tanzania

Naibu waziri  wa mambo ya nje ya  ushirikiano wa  afrika mashariki Dkt Damas Ndumbaro akizungumza na wandishi wa habari kuhusu  wawekezaji kutoka nchini uturuki makampuni saba yatakayokuja nchini  Picha na Omar Fungo

Muktasari:

  • Ujumbe wa  kampuni saba za Uturuki umewasili nchini kwa ziara ya siku sita. Wawekezaji hao watatembelea mikoa ya Dodoma na Simiyu ambako wanatarajia kufanya uwekezaji wao.

Dar es Salaam. Ujumbe wa kampuni saba kutoka Uturuki umewasili nchini Tanzania kwa ziara ya siku sita na wawakilishi wake wanatarajia kuwa na mkutano na wadau mbalimbali sambamba na kutembelea maeneo ya uwekezaji mikoa ya Dodoma na Simiyu.

Kampuni hizo zinatarajiwa kufanya uwekezaji kwa kujenga viwanda vya nguo, sukari, saruji, viwanda vya kuchakata mazao ya kilimo, viwanda vya kutengeneza vifaa vya ujenzi na uwekezaji katika sekta ya nishati.

Akizungumza na vyombo vya habari leo Jumapili Novemba 18, 2018 Naibu Waziri wa Mambo ya Nje, Dk Damas Ndumbaro amesema uhusiano kati ya Uturuki na Tanzania umeimarika zaidi baada ya Serikali kufungua ubalozi nchini humo mwaka 2016.

"Takwimu za mwaka 2017 zinaonyesha kwamba urari wa biashara kati ya Tanzania na Uturuki umeongezeka na umekuwa mzuri kwa upande wetu. Tumenunua kwao bidhaa zenye thamani ya Sh8 bilioni lakini tumeuza bidhaa za Sh149 bilioni, hili ni jambo ambalo hutokea mara chache sana kwa nchi zinazoendelea," amesema.

Dk Ndumbaro amesema wawekezaji hao watakutana kesho na kuzungumza na wadau na siku inayofuata watakwenda Dodoma ambako watafanya uwekezaji wa hoteli zenye hadhi ya nyota tano na maduka makubwa (shopping malls).

Amesema Uturuki ndiyo nchi ya kwanza kuunga mkono Serikali kuhamia Dodoma na wanakwenda kufanya uwekezaji huo wakiamini kwamba kuna fursa kubwa za uwekezaji.

Amesema kampuni hizo zikikamilisha uwekezaji wao watatengeneza ajira zaidi ya 1400 kwa Watanzania. Amesema Waturuki wamepanga kuongeza uwekezaji wao hapa nchini ambao sasa una thamani ya Dola 324 bilioni kutoka katika kampuni 48 ambazo zimeajiri watanzania 3,500.

Kwa upande wake, Balozi wa Uturuki nchini, Ali Dovutoglu amesema ziara ya ujumbe huo itaongeza urari wa biashara kati ya Tanzania na Uturuki.

"Kuna fursa kubwa kwa Watanzania Uturuki hasa kwenye mazao ya kahawa, tumbaku, pamba na korosho. Ushirikiano huu utaimarisha zaidi biashara zetu," amesema.