Kanisa Katoliki DRC lapinga matokeo urais

Muktasari:

Umoja wa Afrika umetoa wito wa kusuluhisha mzozo wowote utakaotokana na matokeo hayo kwa amani na mazungumzo


Kinshasa, DRC. Kanisa Katoliki lenye ushawishi mkubwa nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), limesema kwamba matokeo ya uchaguzi wa rais hayafanani na yale yaliyohesabiwa na wasimamizi wake.

Taarifa ya kanisa hilo iliyotolewa leo imesema matokeo ya uchaguzi huo yaliyotangazwa na tume huru ya uchaguzi, Ceni hayafanani na yale yaliyokusanywa na ujumbe wake.

Kanisa hilo hata hivyo halikusema ni nani linadhani ni Mshindi, lakini duru za kidiplomasia zinasema kanisa linaamini mgombea mwingine wa upinzani, Martin Fayulu ndiye mshindi.

Kiongozi wa upinzani, Felix Tshisekedi mapema leo alitangazwa kushinda uchaguzi wa urais, lakini Fayulu ameyalalamikia matokeo hayo akisema yamechakachuliwa huku akiapa kuyapinga.

Huku haya yakijiri shirika la habari la AFP limesema vikosi vya usalama vimeripoti kuuawa kwa polisi wawili na raia wawili katika maandamano katika mji wa Kikwit, magharibi mwa Congo baada ya polisi kuingilia kati kukomesha maandamano ya kupinga matokeo ya uchaguzi.