Kanyomozi, Zahara waahidi makubwa Vocal Night ya Lady Jay Dee

Muktasari:

Wasanii kutoka nchini Uganda na Kenya, Juliana Kanyomozi , Bulelwa Mkutukana a.k.a 'Zahara' wamesema wataufanya usiku wa Vocal Night kuwa wakukumbukwa Tanzania.


Dar es Salaam. Wasanii kutoka nchini Uganda, Juliana Kanyomozi na Bulelwa Mkutukana a.k.a 'Zahara' kutoka nchini Afrika Kusini wameahidi makubwa katika tamasha la Vocal Night linalotarajiwa kufanyika kesho Oktoba 26 katika Ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari, wasanii hao ambao wamekuja kwa mwaliko wa Lady Jay Dee, wamesema Watanzania watarajie makubwa kwa kuwa wamefanya mazoezi ya kutosha.

Zahara anayetesa na wimbo wa Loliwe, amesema ni wakati pia wa wasanii wachanga na wale wakubwa kukutana katika usiku huu ili kubadilishana mawazo na kuusongesha muziki wa Afrika mbele.

Amesema pamoja na kuwa mara yake ya kwanza kuja nchini, ameuona ukarimu wa watu wa Tanzania na kuahidi kufanya nao kazi za kimuziki.

Wakati kwa upande wa Juliana aliyewahi kutesa na wimbo wa Usiende Mbali na Bushoke, amesema hii sio mara yake ya kwanza kuja nchini kwani amekuwa akifanya kazi na wasanii mbalimbali.

Awali Lady Jay Dee, amesema tamasha hilo litakaloanza saa 3:00 usiku lina lengo la kuonyesha uwezo wa sauti walizonazo wasanii na kutumika kama njia ya kuwainua wengine hususani wasanii wa kike.

"Hakuna asiyejua changamoto tunazopitia wasanii wa kike, lakini usiku wa kesho itakuwa wa kuwaeleza watakaohudhuria namna gani sisi tuliweza kupambana na vikwazo hadi kufika hapa tulipo leo.

Wasanii wengine watakaokuwepo ni pamoja na Grace Matata, Damian Soul huku mgeni rasmi akitarajiwa kuwa Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Juliana Shonza.