Katibu ACT Wazalendo kumshtaki Rais Magufuli, Mwanasheria Mkuu wa Serikali

Muktasari:

Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mawasiliano wa ACT-Wazalendo, Ado Shaibu kumshtaki Rais John Magufuli na Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa maelezo kuwa uteuzi wa mwanasheria huyo hana sifa za kushika nafasi hiyo


Dar es Salaam. Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mawasiliano wa ACT- Wazalendo, Ado Shaibu amempa maelekezo mwanasheria wake, Fatma Karume kufungua kesi Mahakama Kuu kumshtaki Rais John Magufuli na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Dk Adelardus Kilangi.

Akizungumza leo Alhamisi Desemba 13, 2018 jijini Dar es Salaam, Shaibu amesema uteuzi wa AG haukufuata matakwa ya katiba na kwamba Dk Kilangi hana sifa za kushika nafasi hiyo.

Hata hivyo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Amon Mpanju alipoulizwa kuhusu suala hilo amesema hawezi kutoa ufafanuzi kuhusu malalamiko ya Shaibu kwa sababu hajui amesema nini na amelalamika kuhusu sheria ipi iliyokiukwa.

Kwa upande wake Fatma Karume ambaye ni Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) amesema amepokea maelezo ya Shaibu na jana alikwenda kuandikisha shauri hilo Mahakama Kuu.

Katika maelezo yake Shaibu amesema Ibara ya 59 ya Katiba imetaja masharti ya Mwanasheria Mkuu ambayo ni; kwanza, atateuliwa kutoka miongoni mwa watumishi wa umma; pili, mwenye sifa ya kufanya kazi kama wakili; tatu, awe amekuwa na sifa hizo kwa muda wa miaka 15 au zaidi.

"Tangu alipoteuliwa Februari, 2018 nimejipa muda kufanya uchunguzi nikabaini kwamba Dk Kilangi hana hizo sifa zote. Hana sifa za kuwa Mwanasheria Mkuu kwa mujibu wa Katiba," amesema Shaibu.

Amesema amemhusisha Rais Magufuli katika kesi hiyo kwa sababu yeye ndiyo aliyefanya uteuzi huo ambao unakiuka matakwa ya Katiba.

Shaibu amesema katika utafiti wake amebaini kwamba Dk Kilangi amesajiliwa kuwa wakili mwaka 2011, hivyo amefikisha miaka saba kama wakili.

Pia, amebaini kwamba tangu mwaka 2004, amekuwa akifanya kazi kwenye taasisi mbalimbali binafsi ikiwemo meneja programu wa Envirocare, mhadhiri wa muda katika vyuo vya Ruaha na Tumaini, mshauri wa wanafunzi na mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino.