Kigogo wa zamani TRL, wenzake 17 wapandishwa kizimbani

Vigogo wa Shirika la reli Tanzania (TRC) wanaodaiwa kutumia vibaya madaraka yao na kulisababishia shilika hilo hasara kwa kuingia mikataba ya ununuzi wa vichwa vya treni, bila kufanya tathimini ya zabuni na kampuni ya uhandisi na viwanda ya Hindusthan, wakiwa katika mahakama ya mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam leo, wakisubiri kusomewa mashtaka. Picha na mpiga picha wetu

Muktasari:

  • Aliyekuwa mkurugenzi mkuu wa Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) sasa TRC, Kipallo Kisamfu na wenzake 17 wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kusomewa mashtaka 15 ya matumizi mabaya ya madaraka

Dar es Salaam. Aliyekuwa mkurugenzi mkuu wa Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) sasa TRC, Kipallo Kisamfu na wenzake 17 wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kusomewa mashtaka 15 ya matumizi mabaya ya madaraka.

Kisamfu na wenzake ambao ni wahandisi na mameneja wamepandishwa kizimbani leo Jumatano Desemba12, 2018 kwa kuingia mikataba ya zabuni ya ununuzi wa vichwa vya treni na kuipa zabuni hiyo kampuni ya Hindusthan Engineering and Industries Limited

Hayo yameelezwa na mwendesha mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Maghela Ndimbo mbele ya HakimuMkazi Mkuu, Wilbroad Mashauri

Mbali na Kisamfu washtakiwa wengine ni Gilbert Alfred Minja ambaye amesomewa mashtaka bila kuwepo mahakamani pamoja na Paschal John Mafikiri (Kaimu mhandisi mitambo mkuu).

Wengine ni Anthony Emmanuel Munishi (meneja usambazaji) Charles Ndenge (kaimu meneja wa usafirishaji), Ferdinand Soka (kaimu meneja msaidizi wa usambazaji), Muungano Kaupunda (kaimu mkuu wa kitengo cha ufundi).

Joseph Syaizyagi, Kedmond Mapunda, Lowland Simtengu, Ngoso Ngosomwile, Yonah Shija, Malumbo Malumbo, Stephan Kavombwe, Donatus Bandebe, John Charles na Ally Mwangila.

Baada ya kusomewa mashtaka hayo walikana na Hakimu Mashauri kuwataka kila mmoja kuwa na wadhamini watakaokuwa na barua za utambulisho na kusaini bondi ya Sh20 milioni.

Washtakiwa wote walitimiza masharti ya dhamana, kesi hiyo kuahirishwa hadi Januari 18, 2019.