Kikwete awataka wahitimu kujiandaa kisaikolojia

Muktasari:

Rais mstaafu Jakaya Kikwete amewataka wahitimu wa elimu Chuo Kikuu Kishiriki cha Mkwawa kujiandaa kisaikolojia kufundisha shule za msingi bila kujali kiwango cha elimu walichonacho


Iringa. Rais mstaafu Jakaya Kikwete amewataka wahitimu wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Mkwawa kujiandaa kisaikolojia watakapochaguliwa kufundisha shule za msingi.

Ametoa kauli hiyo leo Jumamosi Desemba  8, 2018 katika mahafali ya 10 ya chuo hicho.

Amesema kutokana na elimu na teknolojia kukua nchini Tanzania itawalazimu wahitimu wa elimu kufundisha shule za ngazi  yoyote bila kujali kiwango cha elimu walichonacho.

Kikwete alitoa kauli hiyo akitolea mfano walimu waliokuwa wakifundisha shule za sekondari ambao siku za hivi karibuni walipangiwa kufundisha shule za msingi.

Mmoja wa wahitimu, Venance Peter amesema yupo tayari kufanya kazi sehemu yoyote ili kuhakikisha anakidhi malengo ya Taifa.

"Nimejiandaa kisaikolojia walioathirika mwanzo ni wale walioshushwa bila taarifa lakini mimi nimejiandaa kisaikolojia na ninafurahi kuandaliwa mapema haitaniathiri chochote,” amesema.