Kilichowaachia huru Diane na, mama yake hiki hapa

Muktasari:

  • Jopo la majaji watatu wa Mahakama Kuu ya Rwanda limesema upande wa mashtaka katika kesi iliyokuwa ikimkabili mwanasiasa, Diane Rwigara na mama yake, Adeline Rwigara uliwasilisha ushahidi ambao haukukidhi kuwatia hatiani washtakiwa hao na pasi na shaka hawana hatia.

Kigali, Rwanda. Mahakama Kuu ya Rwanda imewaachia huru mwanasiasa, Diane Rwigara na mama yake, Adeline Rwigara baada ya kuwakuta hawana hatia baada ya upande wa mashtaka kukosa ushahidi wa kutosha katika kesi hiyo.
Wawili hao na wenzao wanne ambao hawakuwapo mahakamani wakati wote kesi hiyo ikiendeshwa, walikuwa wanashtakiwa kwa madai ya kuchochea machafuko miongoni mwa wananchi, kuleta mgawanyiko na ubaguzi na Diane alikabiliwa na shtaka moja zaidi la kughushi nyaraka.
Jopo la majaji watatu wa Mahakama Kuu likisoma hukumu yake lilisema kwamba upande wa mashtaka uliwasilisha ushahidi ambao haukukidhi kuwatia hatiani washtakiwa hivyo hawana hatia.
Wanawake hao ambao wamekuwa nje kwa dhamana walikuwapo katika chumba cha Mahakama kilichokuwa kimejaa watu juzi mchana pamoja na wanasheria wao.
Kwa mujibu wa majaji, kwa kiasi kikubwa kesi hiyo ilikuwa imejengwa kupitia mikanda ya sauti iliyorekodiwa ambayo ilitengenezwa na kusambazwa kwa watu mbalimbali kupitia jukwaa la mtandao wa kijamii wa Whatsapp.
"Hata hivyo, upande wa mashtaka umeshindwa kuthibitisha ni namna gani mikanda hiyo ya kusikiliza inaweza kuchochea watu kwa sababu ilikuwa imeandaliwa kwa ajili ya watu binafsi. Mashtaka halisi yalipaswa yawe njama za kuchochea lakini hayamo kwenye hati ya mashtaka,” majaji walisema.
Shtaka dhidi ya Diane linalohusu kuchochea umma dhidi ya Serikali, waendesha mashtaka walitegemea sehemu za vipande vya habari vilivyoandikwa na waandishi wa habari kwenye mikutano yake katika kipindi cha kuelekea uchaguzi mkuu wa Rais ambao hakupitishwa kugombea mwaka 2016.
Kwa mujibu wa majaji, matamko aliyotoa wakati ule yalikuwa na uwezekano wa kuwa na madhara na ni propaganda hatari ambazo hazikuthibitishwa dhidi ya Serikali. Hata hivyo upande wa mashtaka walishindwa kuonyesha nia ovu ya kuchochea umma.
Kuhusu shtaka la kughushi, Diane alishtakiwa kwa kutia saini feki alipokuwa anakusanya majina ya watu 600 wa kumuunga mkono ili agombee urais. Mahakama, hata hivyo iliamua kwamba hakukuwa na ushahidi unaotosheleza kwamba mshtakiwa alikuwa ameghushi mwenyewe saini.
"Mahakama imebaini japokuwa uhalali wa baadhi ya saini zilizowasilishwa na mshtakiwa ulitiliwa shaka na wataalamu wa uchunguzi wa kimahakama, jukumu lilikuwa la upande wa mashtaka kuthibitisha ushahidi wa saini zilizoghushiwa na mshtakiwa,” inasema sehemu ya hukumu na kuongeza kwamba shaka yoyote kuhusu ushahidi inampa haki mshtakiwa.
"Mahakama kwa hiyo inawaachia huru washtakiwa wote wawili kwa msingi kwamba ushahidi uliowasilishwa na upande wa mashtaka haukuwa unatosheleza."
Hukumu hiyo imelifurahisha shirika la Amnesty International ambalo kupitia Mkurugenzi wa Afrika Mashariki, Pembe na Maziwa Mkubwa, Joan Nyanyuki limetoa wito itumike kujenga msingi wa haki.
"Diane na Adeline Rwigara hawakustahili kushtakiwa kwa kutoa maoni yao. Pamoja na kwamba tunapokea kutolewa na kuachiliwa kwao, tuna wasiwasi kwamba haki ya uhuru wa kujieleza bado inakandamizwa nchini Rwanda," alisema Nyanyuki.
"Tunatoa wito kwa mamlaka ya Rwanda kujenga msingi juu ya hukumu hii na kufanya kazi kuelekea kukuza uvumilivu mkubwa na kukubali maoni mengine na mbadala. Hukumu hii inapaswa kuwa hatua ya kwanza ya kurekebisha mwenendo unaoendelea wa ukandamizaji nchini Rwanda."