Kiluwa: Waziri Lukuvi alinipora fedha

Muktasari:

  • Mohamed Kiluwa, mfanyabiashara anayekabiliwa na kesi ya kutoa rushwa ya Dola 40,000 za Marekani kwa Waziri wa Ardhi, William Lukuvi ameanza kujitetea leo na kueleza kuwa waziri huyo alimpora fedha wakati akiwa ofisini kwake

Dar es Salaam. Mfanyabiashara Mohamed Kiluwa (50) ameieleza mahakama ya Wilaya ya Ilala kuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi alimkaba na kumnyang’anya mkoba uliokuwa na fedha wakati akiwa ofisini kwa waziri huyo.

Kiluwa ameeleza hayo leo Jumatatu Desemba 17, 2018  wakati akijitetea katika kesi ya kutoa rushwa ya Dola 40,000 za Marekani (Sh 90 milioni) kwa Waziri Lukuvi.

Akiongozwa na wakili wa utetezi, Imani Madega mbele ya Hakimu Mkazi, Samuel Obasi, Kiluwa amedai kuwa fedha hizo zilikuwa ni kwa ajili ya ununuzi wa mapazia na jenereta kwa ajili ya ofisi yake aliyokuwa akiiboresha.

“Alinikaba na kuninyang'anya mkoba nilikuwa nimebeba na kisha kuufungua na kutoa fedha zangu ambazo zilikuwa kwa ajili ya kufanya manunuzi ya mapazia na samani nyingine za ndani kwa ajili ya kuboresha ofisi yangu,” amedai.

Kiluwa anajitetea baada ya mahakama kumkuta na kesi ya kujibu baada ya kumkuta na shtaka moja la kutoa rushwa kwa Lukuvi.

Tayari mashahidi sita wa upande wa mashtaka wameshatoa ushahidi dhidi ya Kiluwa, akiwemo Waziri Lukuvi.

Katika ushahidi wake  Lukuvi amedai kuwa alipigiwa simu na msiri wake kuwa kuna fedha chafu kiasi cha dola 40,000 za Marekani zinaletwa ofisini kwake.

Amedai fedha hizo zinapelekwa na Kiluwa ambaye ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Kiluwa Steal Group and Co. Ltd na Kiluwa Free Processing Zone.

Aliieleza mahakama kuwa anatambua kuna mradi wa uwekezaji kwa ajili ya ujenzi wa viwanda uliopo eneo la Mlandizi wilayani Kibaha.

Lukuvi amedai kuwa eneo hilo lina ukubwa wa ekari 1000 na kwamba mmoja wa wamiliki wa mradi huo ni mshtakiwa Kiluwa.

Amedai mshtakiwa aliomba kupimiwa viwanja 73 na kwamba Juni na Julai, 2018 alikuwa amepatiwa hati ya viwanja 57 huku vikibaki viwanja 16 ambavyo vilikuwa havijatolewa hati na msajili.

Alieleza kabla ya kumpa hati hizo 57, Lukuvi alitoa masharti kwa mshtakiwa huyo, kuwa viwanja hivyo viendelezwe ndani ya miaka miwili na asipofanya hivyo atanyang’anywa viwanja kwa mujibu wa sheria.

Lukuvu amedai mbali na kutoa masharti kwa Kiluwa, pia alitoa maelekezo kwa msaidizi wake ambaye ni Kamishana wa Ardhi wa Kanda ya Dar es Salaam, Mathew Nhonge kuwepo na masharti ya kuendeleza eneo hilo ndani ya miaka miwili.

Hata hivyo, Lukuvi amedai kuwa Mathew hakuweka masharti katika hati hizo hali liliyosababisha Lukuvi kumtaka Kiluwa kuwasilisha hati hizo ofisini kwake ili azikague.

Inadaiwa kuwa Julai 16, 2018 katika ofisi za waziri huyo zilizopo Magogoni, Kiluwa alitoa rushwa ya Dola 40,000 za Marekani.

Inadaiwa kuwa mshtakiwa huyo alitoa fedha hizo ili asiwasilishe hati ya umiliki wa viwanja 57 vilivyopo Kitalu B Kikongo na Kitalu D Disunyara katika eneo la viwandani, Kibaha mkoani Pwani.