Kortini kwa rushwa ya Dola 2,000

Muktasari:

  • Meneja wa Fedha wa kampuni mbili za ujenzi, Sureshbabu Kakolu, anatuhumiwa kutoa rushwa ya Dola 2,000 za Marekani (zaidi ya Sh4 milioni) kwa Meneja wa TRA mkoa Kilimanjaro, Msafiri Mbibo ili ampe upendeleo katika msamaha wa kodi ya Sh6.6 bilioni ambayo makampuni yake yanadaiwa.

Moshi. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), imemfikisha kortini meneja wa fedha wa kampuni mbili za ujenzi, Sureshbabu Kakolu kwa tuhuma za kutoa rushwa ya Dola 2,000 za Marekani (zaidi ya Sh4 milioni).

Mshitakiwa huyo alifikisha mahakamani leo Ijumaa Novemba 16, 2018 na kusomewa mashitaka yake mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Mfawidhi wa wilaya ya Moshi, Sophia Masati na kukanusha mashitaka.

Akimsomea kosa lake, mwendesha mashitaka wa Takukuru, Rehema Mteta, amedai Novemba 15, 2018, alitoa rushwa ya kiasi hicho kwa meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoa Kilimanjaro, Msafiri Mbibo.

Fedha hizo ilikuwa ni kishawishi ili meneja huyo apitishe maombi ya msamaha wa kodi ya Sh6.6 bilioni, ambazo kampuni hizo mbili zililimbikiza tangu 2013 hadi Oktoba 2018.

Mshitakiwa huyo anashikilia wadhifa wa Meneja wa Fedha katika kampuni hizo mbili, moja inaitwa Dott Services (TZ) Ltd na nyingine ni General Nile Company for Roads and Bridges/Dott Services JV.