Krismasi imepita Januari hiyo inakuja

Muktasari:

  • Kuikabili Januari, kunahitajika mipango mipya tofauti na mazoea ya miaka iliyo-pita. Katika kipindi hiki ambacho biashara zinakabiliwa na changa-moto nyingi ikiwamo kushindwa kujiende-sha huku kampuni zikipunguza watumishi, kila mmoja anatakiwa kuwa na mkakati wa kutumia vyema anachoki-pata kukidhi mahitaji ya msingi.

Wahenga walisema aliyeng’atwa na nyoka hata akiona jani hushtuka. Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wetu umebaini kuwa wananchi wengi wameufanyia kazi kwa vitendo msemo huu.

Tofauti na miaka ya nyuma ambayo wamekuwa ‘wakijiachia’ kwa kununua mahitaji mengi hivyo kupoteza kiasi kikubwa cha fedha katika sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya, wengi wameshtuka na kuchukua tahadhari wakifahamu fika mlima mrefu wanaokwenda kukabiliana nao Januari, mwezi ambao una rekodi ya kuwa na mahitaji mengi ya lazima kwa familia nyingi.

Ukiwa hutadaiwa kodi ya nyumba, ada za watoto zinakusubiri na hizo ni mbali ya zile za kila mwezi za umeme, maji, leseni mbalimbali na kodi nyinginezo kwa mujibu wa sheria.

Kuepuka madhara ya kutumia fedha nyingi baadhi ya wananchi wamejiwekea mipango kuhakikisha wanafurahia sherehe hizo huku wakiepuka adhabu ya Januari.

Mipango hii ni kwa wote, wateja na wafanyabiashara wa huduma na bidhaa tofauti ambazo zina soko kubwa msimu huu kwa mfano, mkazi wa Goba – Dar es Salaam, Naomi Mosha ameamua kusherehekea Krismasi mwaka huu hapohapo kwake tofauti na miaka ya nyuma ili kuhakikisha kwamba mfuko wake hauyumbi.

Kwa vile ni Mchaga, mara nyingi alikuwa akienda kwao Moshi huku akitumia fedha nyingi kununua mahitaji ya familia yake kama vile nguo na viatu vipya kwa ajili ya watoto, vyakula na vinywaji.

“Mwaka huu tumeamua kusherehekea hapa mjini ili kupunguza gharama. Siku ya Krismasi tulienda kanisani na kurudi nyumbani hatukutaka kuingia gharama za ziada,” alisema.

Alisema amefanya hivyo, kwa sababu familia yake ina mambo mengi ya kufanya Januari. “Ada ndio kipaumbele chetu cha kwanza. Sikukuu zisitufanye tusahau majukumu yetu mengine,” alisema.

Ili kukabiliana na Januari, mchumi na mtafiti mwandamizi wa Repoa, Dk Donald Mmari ameshauri kuwa ingawa kusafiri ni utamaduni wa baadhi ya jamii nchini, ni jambo jema kuangalia bajeti iliyopo ili kuepuka matumizi yasiyo ya lazima.

“Tunaweza kusherehekea bila kunywa na kulewa kwani licha ya kuepuka kutumia fedha nyingi, tutapunguza ajali na kufanya vitendo visivyo vya kistaarabu vitokanavyo na ulevi,” alisema Dk Mmari.

Mkazi wa Mikocheni, Dar es Salaam, Glory Msuya pia alipanga kwenda kusherehekea Krismasi kijijini kwao mkoani Kilimanjaro. “Ni kawaida yetu kusafiri nami hufanya hivyo kila mwaka, lakini nimejifunza kubana matumizi.”

Kutekeleza hilo, alisema badala ya kupanda ndege kwenda na kurudi ambayo angelipa Sh500,000 aliamua kutumia basi hivyo kuokoa zaidi ya Sh400,000 akisema gharama yake ni Sh72,000 tu.

Alisema lazima aondoke Dar es Salaam msimu huu kwa kuwa huwa anapaona pamejaa na hufurahi zaidi kuumaliza mwaka akiwa nje ya mji, mahali penye utulivu akijumuika na familia yake kijijini.

Mikakati ya shule

Kuhakikisha kuwa wazazi hawashindwi kulipa ada na gharama nyingine, shule nyingi zimeandaa mikakati mbalimbali kuwasaidia.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Patmo Junior, Charles Malango alisema, menejimenti imekuwa ikiwataka wazazi kulipa ada kuanzia Oktoba.

“Tunawapa muda wa kutosha kulipa gharama za shule kwa kuwa tunafahamu huwa wanajisahau kipindi cha Krismasi na Mwaka Mpya,” alisema.

Alisema hatua hiyo imetokana na wazazi au walezi wengi kwenda shuleni baada ya sikukuu kuomba waongezewe muda wa kulipa ada kwa mwezi mmoja au miwili zaidi.

“Tunataka ada ilipwe kabla ya sikukuu kuepuka matatizo kama hayo kwa sababu watu wengi huwa hawapangilii mambo yao hivyo kutumia fedha zote Desemba,” alisema.

Kupanga kabla

Kuonyesha mfano, Mwalimu Malango aliyesafiri na familia yake kwenda Mbeya alisema alianza kutunza fedha tangu Desemba mwaka jana.

Alisema alikuwa anaweka Sh50,000 kila mwezi na alitumia mshahara wake wote wa Oktoba kwa ajili ya safari hiyo.

“Sikusafiri mwaka 2016 na 2017 kwa kuwa nilikuwa na mambo mengine muhimu. Kipindi hicho nilikuwa nasoma. Sitarajii kusafiri tena miaka miwili ijayo kwa vile ninayo malengo ya kufanikisha,” alisema.

Meneja wa Shule za Elite Sprints, Elizabeth Fuime alisema naye huweka mipango kabla ya msimu wa sikukuu pia. Alisema hununua mahitaji yote muhimu kabla kwani bei huwa nafuu tofauti na kipindi cha sikukuu za mwisho wa mwaka ambacho gharama huongezeka.

Mapato ya wafanyabiashara

Wakati mbinu hizi za kubana matumizi zikionekana kuwa mkombozi kwa wateja wa huduma na bidhaa mbalimbali, hali ni tofauti kwa wafanyabiashara ambao hutegemea kutengeneza fedha za kutosha.

Mfanyabiashara ya duka eneo la Mwenge, Dar es Salaam, Halfan Mundamo alisema mambo yamebadilika kiasi kwamba ana shaka kama atamudu kulipa ada na gharama nyingine za shule kwa wakati.

Alisema zamani alikuwa anauza mpaka Sh500,000 kwa siku kwenye msimu wa sikukuu hizi mwaka huu akiingiza Sh100,000 ni bahati.

“Biashara haiendi vizuri kwa kweli. Wateja wamepungua sana ikilinganishwa na miaka ya nyuma. Watu wanabana sana matumizi. Tulikuwa tunategemea mauzo ya msimu huu kulipa ada lakini sifahamu itakuwaje hapo Januari,” alisema.

Mfanyabiashara mwingine wa Mwenge, Adela Kanje alisema zamani baadhi ya watu walikuwa wakinunua kilo 200 za mchele lakini sasa hivi, kiasi kikubwa ni kilo 50.

Kwa kipindi hicho, alisema mauzo yalikuwa yanaanza kuimarika kuanzia Desemba 15 lakini mwaka huu, hadi Desemba 18 mambo yalikuwa hayaeleweki.

“Watu hawana fedha nyingi za kutumia kama ilivyokuwa awali. Mpaka sasa wanakuja wateja wa kawaida, wale wa siku zote tu,” alisema Adela.

Sio chakula na mavazi pekee, hata mapambo na zawadi za sikukuu nazo hazikuwa kama zamani. Mfanyabiashara wa bidhaa hizo, Sayuni Kawerd alisema kwa uzoefu wake wa miaka saba kwenye biashara hiyo, mwaka huu mambo yameenda kombo kwa kiasi kikubwa.