Kunguru walivyovamia ndege ya Precision

Muktasari:

  • Shirika la Ndege la Precision limeeleza jinsi ndege yake aina ya PW 722 ilivyopata hitilafu wakati  ikitua katika Uwanja wa Ndege wa Mwanza baada ya kuvamiwa na kundi la ndege

Dar es Salaam. Shirika la Ndege la Precision limeeleza jinsi ndege yake aina ya PW 722 ilivyopata hitilafu wakati  ikitua katika Uwanja wa Ndege wa Mwanza baada ya kuvamiwa na kundi la ndege.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Jumatatu Desemba 10, 2018 inaeleza kuwa ndege hiyo ilikuwa ikitokea Nairobi, Kenya kupitia Kilimanjaro na kisha Mwanza ikiwa na abiria 68 pamoja na wafanyakazi wanne.

Inaeleza kuwa wakati ikiwa katika harakati za kutua ilivamiwa na ndege hao hali iliyomfanya rubani kutumia ujuzi kuhakikisha inatua salama.

“Timu ya wahandisi  inafanya tathmini na ukaguzi ili kushughulikia tatizo lililojitokeza. Mabadiliko ya kusogeza mbele ratiba za ndege zake yanatakiwa kufanyika. Tutahakikisha tunaepuka athari na usumbufu wowote kwa wateja wetu ili kufanikisha safari zao,” inaeleza.

“Abiria wote watakaoathiriwa na mabadiliko ya ratiba za safari hizo watapewa maelekezo. Kwa sasa  wataalamu wetu wanaendelea na jitihada za kuhakikisha wanapunguza muda wa ratiba za kusubiri zaidi.”

Picha za ndege hiyo jana zilisambaa katika mitandao ya kijamii, zikionyesha sehemu moja ya tairi ikiwa imepata hitilafu baada ya ndege hao kunasa.