Kushamiri usafiri wa bajaji, kilio kwa wenye dadalada Moshi

Ongezeko la bajaj katika Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro, Desemba 3, 2018 lilitikisa mjini huo baada ya madereva wa daladala kugoma kutoa huduma kushinikiza bajaji hizo zisiruhusiwe kusimama na kupakia abiria kwenye vituo vya daladala.

Daladala ambazo ziligoma kutoa huduma ni zile zinazofanya safari zake kati ya mji wa Moshi, Pasua, Majengo, Soweto na KCMC.

Mgomo huo ambao ulidumu kwa siku tatu na kusababisha athari mbalimbali kwa wananchi wakiwamo wafanyakazi, wanafunzi na wafanyabiashara ambao walishindwa kutekeleza majukumu yao katika utaratibu wa kawaida.

Mgomo huo pia ulisababisha nauli ya bajaji kuongezeka kutoka Sh500 iliyokuwa ikitozwa awali kwa abiria mmoja hadi Sh1,000 kwa safari moja kwa kila abiria.

Wananchi walilazimika kukodi bodaboda na wengine kutembea kwa miguu. Kwa kifupi kila mmoja alitafuta namna ya kumfikisha alikotaka kwenda ama kikazi au kwa ajili ya shughuli za kijamii.

Lawama nyingi zikaelekezwa kwa Manispaa ya Moshi na Sumatra zikilalamikiwa kushindwa kusimamia sheria, utaratibu na hivyo kutotimiza wajibu wao.

Wakizungumzia mgomo huo kwa nyakati tofauti, wananchi wa Moshi walieleza kuwa miongoni mwa athari zake ni watu wengi kushindwa kufika katika maeneo ya kazi kwa wakati na wanafunzi kufika shuleni kwa muda stahili.

Jackline Mroso, ambaye ni wa mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Majengo anasema kutokana na mgomo huo ilimlazimu kutembea kwa miguu kwenda na kurudi shuleni wastani wa kilomita 10 kila siku.

“Kabla ya mgomo nilikuwa nikipanda daladala kwa Sh200, madereva walipogoma bajaji nazo zilikataa kutusafirisha wanafunzi kwa nauli hiyo, ikawa hakuna namna nyingine zaidi ya kutembea kwa mguu kazi ambayo haikuwa rahisi hata kidogo,” anasema.

Anaongeza; “Wanafunzi tuliathirika zaidi maana baadhi tulilazimika kutembea kwa saa mbili au zaidi kwenda shuleni, ukifika unakuwa umechoka hata kile ambacho mwalimu anakifundisha darasani huwezi kukielewa.”

Mmoja wa wafanyabiashara wa eneo la Msaranga, Agatha Joseph anasema wakati wa mgomo huo alishindwa kwenda sokoni kununua bidhaa kwa ajili ya genge lake.

“Nilizoea kuamka saa 11 alfajiri kwenda Mbuyuni kununua vitu vya gengeni, lakini siku zote za mgomo nilishindwa kwa sababu kukodi bodaboda gharama ni kubwa ambazo haziwezi kujilipa katika biashara,” anaeleza Agatha.

Anaongeza; “Wafanyabiashara waliokubali kuingia gharama zaidi kwa kukodi bodaboda nao walipandisha bei za bidhaa. Hata hivyo ilikuwa ni hasara kwa kuwa wateja walishindwa kumudu bei bidhaa zikadoda”.

Mkazi wa KCMC maeneo ya Usharika wa Neema, Adolfina Laswai anaeleza kuwa, mgomo huo ulisababisha usumbufu mkubwa katika barabara ya KCMC kutokana na misururu ya watembea kwa mguu waliosindwa kusafiri kwa daladala au bajaji.

“Nashughulika katika mgahawa, tunapaswa kuingia kazini saa 12 asubuhi, lakini siku ya kwanza ya mgomo nilichelewa nikaingia saa mbili. Nilipofika bosi wangu aliniambia nirudi nyumbani nikapumzike hadi atakaponiita, niliumia maana nilihisi nitafukuzwa kazi,” anaeleza.

“Sumatra na Manispaa wafanye kazi zao ipasavyo wasiishie kutoa maagizo tu wananchi tunataabika maana wakati mwingine mfukoni unatembea na Sh1,000 tu, hivyo unapotokea mgomo kama huu fedha hiyo haikufikishi nyumbani,” anasema.

Madereva wa daladala wazungumza

Mmoja wa madereva wa daladala zinazofanya safari kati ya Moshi mjini na Pasua, Jackson Kinyaiya aliliambia Mwananchi kuwa changamoto waliyonayo ni viongozi wa Sumatra kushindwa kutatua tatizo la bajaji kuwaingilia katika vituo vyao na kupakia abiria.

“Hawa bajaji wamekuwa wakiingia katika maeneo yetu, tumepeleka malalamiko kwa viongozi husika lakini hakuna ufumbuzi uliochukuliwa tumeamua kugoma ili tupate mwafaka wa jambo hili,” anasema Kinyaiya.

Sanael Mushi, dereva daladala kati ya Moshi mjini na KCMC anaituhumu Sumatra kuwa chanzo cha mgomo huo kwa kushindwa kutoa utaratibu unaoeleweka kwa bajaji ili kuepusha kuingiliana na daladala wakati wa kuendesha shughuli zao.

“Wapo baadhi ya viongozi wana maslahi katika hili, ndio maana tumezunguka ofisi zote bila kupatiwa ufumbuzi. Tunashindwa kufanya kazi na bajaji, wamekuwa kero kubwa kwetu. Wanasababisha tulio katika biashara ya daladala tunashindwa hata kulipa kodi kwa sababu hatuingizi faida,” anasema Mushi.

Naye Hussein Ally, dereva daladala Soweto, anasema wameamua kurudisha funguo za magari kwa wamiliki kwani wamekua wakifanya kazi bila faida. “Abiria wote wanachukuliwa na bajaji”.

Naye kiongozi wa daladala Mjini Moshi, Kennedy Mlack anasema kuwa, bajaji zimekuwa zikifanya kazi kama daladala hali ambayo inazifanya daladala zikose abiria na mapato kwa ajili ya kuilipa manispaa.

Kiongozi wa daladala zinazofanya safari kati ya Moshi Mjini na KCMC, Ibrahim Mzava anasema baada ya kukaa pamoja na uongozi wa Manispaa na Sumatra walikubaliana kuziondoa bajaji hizo.

“Ahadi za Manispaa zimekua hazitekelezeki, awali walituambia baada ya kile kikao watapita na gari la matangazo kuondoa bajaji hizo mjini, lakini hadi sasa hakuna kinachoendelea, hivyo tumeamua kupaki hatufanyi kazi mpaka kieleweke,” anasema Mzava.

Maelekezo kwa bajaji

Katibu wa Waendesha Bajaji Mkoa wa Kilimanjaro, Rashid Omary aliwataka madereva hao kufuata sheria zilizowekwa na Sumatra kwa kila mtu kukaa eneo analostahili kulingana na kile anachoelezwa katika leseni yake.

“Nchi hii ina utaratibu, niwaombe vijana wangu wafuate sheria zilizowekwa kwenye lesini zao ili waondokane na migogoro ya mara kwa mara,” anasema.

Kwa upande wake, Meya wa Manispaa ya Moshi, Raymound Mboya anasema Mji wa Moshi ni mdogo, hivyo kinachopaswa kuzingatiwa ni busara na namna ya kukabiliana na hali hiyo. Kusema bajaji ziondoke katikati ya mji ni kitu kisichowezekana.

Kauli ya Mkurugenzi

Akijibu malalamiko ya madereva hao, Mkurugenzi wa Manispaa ya Moshi, Michael Mwandezi aliwataka madereva hao kuendelea na kazi mpaka mkuu wa Mkoa atakaporudi ili wakae meza moja kujadili jambo hilo.

“Kuhusu kuwaondoa bajaji katikati ya mji hilo ni gumu, endeleeni kufanya kazi mengine tutaendelea kuyashughulikia. Mkuu wa Mkoa akija tutakaa meza moja ili tutatue tatizo hili,” anasema.