Kwa nini korosho zina kelele kila msimu?

Muktasari:

Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazolima kwa wingi zao la korosho ambapo kwa Afrika inashika nafasi ya nne huku kidunia ikiwa ni ya nane.

Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazolima kwa wingi zao la korosho ambapo kwa Afrika inashika nafasi ya nne huku kidunia ikiwa ni ya nane.

Nchi nyingine zinazolima korosho kwa wingi duniani ni Brazil, India, Vietnam, Ghana, Ivory Coast, Msumbiji na Burkina Faso.

Korosho ndilo zao linaloongoza kuiingizia Tanzania fedha za kigeni kuliko mazao mengine ya biashara kama pamba, kahawa, karafuu na chai.

Uzalishaji wa korosho nchini umekuwa ukipanda na kushuka tangu zilipoanza kulimwa nchini, lakini kwa miaka ya hivi karibuni uzalishaji umekuwa ukipanda.

Kutokana na umuhimu wa zao hilo, mwaka huu Serikali imeingilia soko lake kwa kununua korosho za wakulima kwa Sh3,300 baada ya wakulima kuwagomea wafanyabiashara waliotaka kununua bei ya juu Sh 2,700 na bei ya chini ya Sh1,700 wakati katika msimu wa mwaka jana korosho ziliuzwa kwa bei ya juu hadi Sh4,000 kwa kilo moja.

Kwa mara ya kwanza pia Serikali imeliagiza Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kusimamia usafirishaji, ubanguaji, ununuzi pamoja na mauzo ya korosho.

Historia

Profesa Peter Massawe ambaye ni mtafiti kiongozi wa korosho katika kituo cha utafiti wa Kilimo cha Naliendele mkoani Mtwara, anasema zao hilo lenye historia ndefu limeipa heshima Tanzania kwa kuongoza katika tafiti duniani.

“Korosho zililetwa na Wareno katika karne ya 16, kama zao la kuzuia mmomonyoko wa udongo na si zao la biashara. Hata hivyo, baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia zao hilo lilianza kupata umaarufu, ambapo tani 7,000 zilisafirishwa kwenda India,” anasema Profesa Massawe.

“Uzalishaji uliendelea kuongezeka nchini kwa kasi kubwa ambapo katika msimu wa mwaka 1973 ulifikia tani 145,000 na kuifanya Tanzania kuwa ya pili duniani kwa uzalishaji ikitanguliwa na Msumbiji.”

Anasema ni wakati huo ambapo viwanda 10 vya kubangua korosho vilijengwa nchini baada ya Serikali kupata mkopo kutoka Benki ya Dunia. Katika kipindi hicho korosho duniani zilikuwa zinasemekana ni zao lisilokuwa na magonjwa wala wadudu hatarishi hivyo hata uwekezaji katika utafiti ulikuwa mdogo ukilinganisha na kahawa, chai, pamba au katani.

Hata hivyo, anaitaja sera ya vijiji vya ujamaa iliathiri uzalishaji wa zao hilo ambao ulishuka na kufikia tani 16,400 mwaka 1986.

“Wananchi walihamishwa kutoka maeneo yao ya asili na kwenda katika vijiji vipya na kuyatelekeza mashamba yao. Hali hiyo ilisababisha kuenea kwa magonjwa na wadudu hatarishi wa korosho,” anasema.

Ni wakati huo ambao Profesa Massawe anasema Serikali iliingilia kati na kuanzisha mradi mdogo wa kutathmini sababu za kushuka uzalishaji wa zao hilo ambao ulifanyiwa kazi kuanzia mwaka 1985 hadi 1989 (Cashew Production, Improvement Pilot Project (CPIPP).

Anasema tathmini hiyo ilifuatiwa na mradi wa uendelezaji zao la korosho (CIP) mwaka 1990 hadi 1996 uliofadhiliwa na Benki ya Dunia, Serikali ya Uingereza kupitia ODA (Sasa DFID).

“Mradi huo uliimarisha utafiti wa korosho kwa kusomesha watafiti hadi shahada ya uzamivu (PhD), kuboresha mazingira ya kufanyia kazi, vitendea kazi na usambazaji wa teknolojia mbalimbali,” anasema.

Kutokana na maboresho hayo, anasema uzalishaji uliongezeka kutoka tani 17,059 mwaka 1989/90 hadi tani 100,000 mwaka 1998/99 na bei ilitoka Sh250 kwa kilo moja hadi Sh800 kwa kilo.

Bodi ya Korosho Tanzania

Zao la korosho linadhibitiwa na Bodi ya Korosho Tanzania (CBT) iliyopitia mabadiliko mbalimbali ya kisheria yanayoendana na majukumu yake. Mwaka 1962 ilikuwa ikiitwa Southern Region Cashewnut Board na 1963 ilibadilishwa kuwa Southern Agricultural Products Board, kabla ya kuwa National Agricultural Products Board mwaka 1964.

Mwaka 1973 ilibadilishwa kuwa Cashewnut Authority of Tanzania (Cashewnut Industry Act 1973), kabla ya kuwa Tanzania Cashewnut Marketing Board baada ya kubadilishwa kwa sheria Na. 21 ya 1984.

Mwaka 2009 ikawa Cashewnut Board of Tanzania.

Faida za korosho

Kwa mujibu wa mtandao wa Focus Media, korosho zina faida 15 mwilini ikiwamo kuimarisha afya ya moyo kwa kuupa nguvu kuimarisha misuli yake na hivyo kuuepusha kupanuka.

Pia, zinasaidia katika kuundwa kwa seli nyekundu za damu na humkinga mtu dhidi ya ugonjwa wa kisukari, upungufu wa damu pamoja na vidonda vya tumbo.

Korosho pia zina protini na madini muhimu ambayo ni shaba, kalsiamu, magnesiamu, chuma, fosforasi, potasiamu, zinki na sodiamu ingawa iko kwa kiasi kidogo na magnesiamu ambayo ni muhimu kwa afya ya mifupa. Korosho hasa za Tanzania zina vitamini C, vitamini B1, vitamini B2, vitamini B3, vitamini B6, folate, vitamini E na vitamini K.

Mafuta ya korosho hupunguza viwango vya cholesterol HDL, viwango vya triglyceride pia hupunguza shinikizo la damu.

Korosho zina madini ya zinki ambayo yanaimarisha mfumo wa kinga dhidi ya maambukizi ya microbial, protini na uponyaji wa majeraha. Ni muhimu zaidi wakati wa ujauzito na katika ukuaji wa mtoto.

Nini kifanyike kuinua zao la korosho?

Katika kupunguza au kumaliza matatizo na kelele za mara kwa mara katika zao hili, mhadhiri wa uchumi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Haji Semboja anashauri Serikali kuuangalia mfumo wa uzalishaji korosho tangu kilimo hadi masoko na kufanya marekebisho.

“Tusizungumzie tu korosho, bali tuangalie mfumo mzima wa kilimo hadi biashara yake. Tatizo la mazao haya ya biashara hasa kwa nchi masikini ni kutokuwa na msimamo kwenye masoko. Wakulima wadogo wanavuja jasho, lakini inabidi kuangalia mwenendo wa soko na tabia zake,” anasema Dk Semboja.

Dk Semboja pia ameitahadharisha Serikali kwa hatua yake ya kutaka kubangua korosho zote kabla ya kuuza akisema ni suala lililopitwa na wakati.

“Hii hadithi ya kutaka kubangua korosho ni ya kale. Tatizo la Tanzania ni kutojifunza kwa yaliyopita, huwezi kusema unabangua korosho kwenye viwanda vilevile vya zamani visivyo na usafi unaotakiwa. Mwalimu Nyerere alitaka kubangua korosho kwa viwanda hivi ilishindikana.

“Viwanda vya sasa viko chini ya sera ya mwaka 1996, kwa mtazamo wangu tusipoangalia tutarudi kwenye uzalishaji wa mwaka 1973 kwa sababu viwanda vimepitwa na wakati,” anasema.

Anashauri biashara hiyo iachwe kwa watu binafsi wenye masoko yao nje ya nchi na wenye taarifa za kutosha bila kutegemea Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji.