VIDEO: Lema anavyotumia mitandao ya kijamii kufikisha ujumbe

Muktasari:

  • Unaweza kusema mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema anatumia mitandao ya kijamii kama fursa ya kufikisha ujumbe kwa jamii

Dar es Salaam. Unaweza kusema mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema anatumia mitandao ya kijamii kama fursa ya kufikisha ujumbe kwa jamii.

Huenda hiyo inatokana na zuio la wanasiasa kufanya mikutano ya hadhara, sasa Lema anaona mitandao hiyo ni njia muafaka kutoa dukuduku lake moyoni kuhusu masuala mbalimbali yanayotokea nchini Tanzania.

Karibu kila tukio kubwa linalotokea  Lema haliachi likapita hivi hivi, lazima aliweke katika mtandao wa kijamii na kuwafanya watu wa kada mbalimbali kutoa maoni yao wakipinga na wengine kupongeza.

Baadhi ya hoja za Lema mtandaoni ni pamoja na sakata la ununuzi wa korosho, tukio la kutekwa kwa mfanyabiashara Mohamed Dewji ‘Mo’, sakata la ushoga lililoibuliwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.

Mara kadhaa mbunge huyo amekuwa akiwashauri viongozi wa Serikali kupitia mtandao hiyo jinsi ya kufanya mambo mbalimbali baada ya wanayokuwa wameyafanya wakati husika kuibua hali ya sintofahamu.

Mathalani katika sakata la kuporomoka kwa bei ya zao la korosho na uamuzi wa Serikali kununua korosho hizo Lema aliweka kauli za viongozi wa Serikali walizozitoa kuhusu uamuzi huo akishauri kuhusu jambo hilo.

“Mheshimiwa Mbowe (Freeman- mwenyekiti wa Chadema)  na mbunge Easter Matiko wako mahabusu. Mahakama inapaswa kujiondoa katika mkakati huu unaofanywa na mawakili wa Serikali wa kushambulia haki. Jaji Mkuu anapaswa kuingilia kati na mahakama ya rufaa kuitisha jalada haraka la kesi hii. Ukimya ni hatari kwa uhuru wa Mahakama,” aliandika Lema akizungumzia kukwama kwa rufaa ya viongozi hao wawili.

Matukio ya watuhumiwa kukamatwa na polisi na kuonyeshwa hadharani  kama anavyofanya kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Gilles Muroto pia humuibua Lema mara kwa mara akilaani jambo hilo kuwa ni sawa na kuwahukumu watuhumiwa.