VIDEO: Lindi nao kuunganishiwa gesi asilia majumbani

Mbunge wa kuteuliwa (CCM), Salma Kikwete akiuliza swali la nyongeza kwa wizara ya nishati, kuhusu wakazi wa Lindi kurukwa na mpango wa usambazaji wa gesi katika makazi yao, wakati wa kipindi cha maswali na majibu bungeni jijini Dodoma leo. Picha na Ericky Boniphace

Muktasari:

Serikali imepanga kusambaza umeme kwenye nyumba za mikoa ya Dar es Salaam, Mtwara na Pwani lakini leo imesema itafanya hivyo pia kwa mkoa wa Lindi

Dodoma. Ingawa hapakuwa na mpango huo, lakini Serikali ya Tanzania imesema itaanza kusambaza miundombinu ya gesi asilia kwa matumizi ya majumbani mkoani Lindi mwishoni mwa mwezi huu wa Mei.

"Aprili 30 utandazaji wa miundombinu utaanza mkoani Mtwara na Mei 30 utaanza mkoani Lindi," amesema Waziri wa Nishati, Dk Medard Kalemani leo Jumanne Aprili 30 alipokuwa anajibu swali la Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Salma Kikwete aliyehoji kwa nini Lindi imerukwa kwenye mpango wa kusambaza gesi hiyo kwa wananchi.

Msingi wa swali la Mama Salma ulitokana na maelezo ya naibu waziri wa wizara hiyo, Subira Mgalu aliyesema Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) linaendelea na ujenzi wa miundombinu ya usambazaji wa gesi majumbani katika mikoa ya Mtwara, Dar es Salaam na Pwani.

Mgalu alikuwa anajibu swali la Mbunge wa Newala Vijijini, Rashid Akbar aliyetaka kujua kwa nini wananchi wa Mtwara  wasiunganishiwe gesi asilia kwenye nyumba zao.

Alisema ununuzi wa mabomba, mita za kupimia gesi na vifaa vya kupunguza mgandamizo wa gesiv inaendelea kuandaliwa ili kutekeleza awamu ya kwanza ya kuziunganisha nyumba 120 mkoani Mtwara hadi mwishoni mwa Juni.

Akiuliza swali la nyongeza, Mama Salma alihoji: "Kwenye mpango wa kusambaza gesi majumbani Lindi imerukwa, ni lini nyumba za wananchi wa Lindi zitaunganishwa na gesi asilia?"