Lukuvi alivyoacha vumbi K’njaro

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Moshi mkoa wa Kilimanajaro katika programu ya Funguka kwa Waziri ambapo wananchi waliwasilisha kero mbalimbali za ardhi kwa lengo la kutafutiwa ufumbuzi.

Muktasari:

  • Moja ya mambo yaliyogusa wengi katika ziara ya Waziri Lukuvi ni pale alipozitaka halmashauri zote Kilimanjaro kutenga maeneo ya umma kwa ajili ya mazishi ili kuondokana na desturi ya kuzika kwenye vihamba agizo ambalo limeacha mjadala mzito huku baadhi ya wananchi wakidai kuwa halitekelezeki.


Moshi. Ziara ya siku mbili ya Waziri Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi katika Wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro, imeacha mtikisiko huku vumbi lake likiendelea kutimka.

Katika siku ya kwanza ya ziara hiyo, Novemba 14 Waziri Lukuvi alitembelea ofisi ya ardhi katika Manispaa ya Moshi na siku iliyofuata alisikiliza kero za migogoro ya ardhi kutoka kwa wakazi wa wilaya hiyo.

Suala ambalo bado linagonga vichwa vya wakazi wa mkoa huo ni agizo lake la kuzitaka halmashauri zote za Mkoa wa Kilimanjaro kutenga maeneo ya umma kwa ajili maziko ili waondokane na desturi ya kuzika kwenye vihamba.

Mazishi kwenye vihamba

Akiwa katika Manispaa ya Moshi, waziri huyo alisema kutengwa kwa maeneo hayo kutaongezea thamani ardhi ambazo wananchi wanazimiliki kimila.

Alifafanua kuwa huenda ni kutokana na halmashauri kutotenga maeneo ya umma ya kuzikia, ndio sababu wakazi wa mkoa huo wameendelea na desturi ya kuzika kwenye vihamba vyao.

Hata hivyo, kauli ya waziri Lukuvi imeonekana kuwasha moto na kuibua mijadala mikali katika mitandao ya kijamii na miongoni mwa wenyeji wa mkoa huu, wengi wao wakisema agizo hilo halitekelezeki.

Mkazi wa Marangu, Moshi Vijijini, Amos Mosha alisema agizo la waziri halitafanikiwa kwani hiyo ni mila na desturi za Wachaga.

“Hicho kitu hakipo kabisa na wala malengo yake hayatafanikiwa. Huwezi kuniambia nisizikie nyumbani kwangu wakati babu na bibi wote wamezikiwa kwenye mashamba ya familia kwanza alama za makaburi zipo na haziwezi futika. Hiyo thamani ya mashamba anayotaka ni yapi wakati tayari tumeshazika?”

Adelard Urassa alisema agizo la kutozika kwenye vihamba ni la kusadikika kwani vijijini hakuna utaratibu wa kupimiwa maeneo na kumtaka waziri Lukuvi akajipange upya.

“Hili suala la kusema halmashauri zitenge maeneo kwa ajili ya kuzikia bado halijaniingia akilini, wangeanza tangu enzi za mababu na mababu wangefanikiwa lakini kwa sasa ni ngumu,” alisema.

Mkazi wa Rombo, Denis Njau alisema agizo hilo linawenda kinyume na mila zao.

Wakati wakazi hao wakisema hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Moshi, Michael Mwandezi alisema maagizo hayo ya waziri yamekuja wakati muafaka na tayari walishanunua eneo jipya katika Kijiji cha Mtakuja kwa ajili ya maziko.

Meya wa manispaa hiyo, Raymond Mboya alisema wamelipokea agizo la waziri kwa mikono miwili na jambo la msingi ni upatikanaji wa maeneo hayo.

Kuhusu migogoro ya Ardhi

Kama ilivyo katika mikoa mingine, Lukuvi alikutana na wananchi wapatao 200. Kundi kubwa lilikuwa la wananchi wa Pasua Block JJJ, ambao waligawiwa viwanja na Serikali lakini wakawekewa alama X.

Baada ya Diwani wa Bomambuzi (CCM), Juma Raibu kuwasilisha kilio hicho, waziri waziri kuahidi kurudi kulishughulikia.

Lukuvi aliagiza viongozi na watendaji wa ardhi kote nchini, kuondoka maofisini na kwenda kusikiliza kero za wananchi huko waliko.

“Nimeagiza, viongozi wasisubiri ninyi muende kwao, nataka wao wawafuate ninyi (wananchi) ,kwani kila wiki lazima wajipange kwenda katika kata na mitaa kusikiliza kero za wananchi”

“Hawa wanachanga fedha zao mnalipwa mishahara, hivi nauli wanapata wapi ya kuwafuata ninyi ofisini?. Lazima maofisa wa ardhi wote wahame maofisini na kwenda kusikiliza wananchi mitaani”.

Mkazi wa Moshi, Serve Kessy alisema kama viongozi kuanzia ngazi ya chini hadi mkoa wangefuata nyayo za Waziri Lukuvi badala ya kumsubiri yeye, ni wazi migogoro ingepata ufumbuzi mapema.

“Hakuna aliyesikilizwa na Waziri siku ile akaacha kufurahi.Nnashauri watendaji kila mmoja awajibike katika kutekeleza majukumu yake.Watoke maofisini waende mitaani,”alidai Kessy.

Ukwepaji kodi ya Ardhi

Baada ya kutembelea ofisi ya Ardhi Manispaa ya Moshi, Lukuvi alidai kugundua baadhi ya mambo ikiwa ni pamoja na uzembe wa watendaji katika kuhudumia wananchi na ukwepaji kodi .

“Kwa hiyo watendaji hawafanyi kazi, lakini pia wananchi wa Moshi mjini, hawapendi kulipa kodi. Tambueni kuwa si hiari yenu kulipa kodi. Wote mlio na viwanja ni lazima mlipe kodi” alisema.

“Moshi inaongoza kwa kutokulipa kodi ambapo katika kipindi cha mwaka jana, waliolipa kodi ya ardhi ni chini ya asilimia 50. Hatuwezi kwenda hivi. Ikifika Februari 2019 tutashughulika nao mahakamani”.

“Eneo lote la moshi limeendelezwa, lakini hamlipi kodi na Moshi ndiyo inaongoza kwa kutokulipa kodi. Mnatakiwa kulipa zaidi ya Sh2Bilioni lakini hamkufika hata Sh1Bilioni mwaka jana,”.

Akizungumza Mkurugenzi wa Manispaa ya Moshi,Michael Mwandezi,anasema tatizo la kutolipwa kodi, linatokana na wananchi walio wengi wa Moshi kuishi nje ya mji huo.

Alisema vianja vingi vya Moshi vimepimwa na wananchi wa Moshi ni walipaji wazuri na kwamba wamekuwa wakilipa kwa mkupuo kipindi cha mwisho wa mwaka ambacho ndicho hurejea.

“Wahusika hawaishi hapa na ndio maana ulipaji wao unakuwa wa mkupuo, na mwisho wa mwaka ndio watu wanakuja na huwenda wakarekebisha mambo yao”anasema

Hati 5,000 hazijachukuliwa

Katika ziara hiyo, Waziri Lukuvi aligundua kuwa wapo watu 5,000, ambao wamepimiwa maeneo yao, lakini hawajachukua hati,huku watu wengine wakiandika barua manispaa na kutojibiwa kwa miaka 18.

“Wenyewe wanasema yapo maeneo watu 5,000,hawajachukua hati. Hili halijawahi kutokea mahala popote kwamba watu wamepimiwa halafu hawajapewa hati zao”alisema Lukuvi na kuongeza kuwa:

“Watu wanaandika barua Manispaa, lakini hawajibiwi kwa miaka 18. File (majalada) hazijafungwa zipo lakini hazisomwi na maofisa wapo pale wanalipwa mshahara. Hili Halikubaliki”

Aidha alisema aligundua tatizo lingine kwamba, wananchi ambao wamepimiwa viwanja vyao Moshi mjini hawapendi kuchukua hati kwa sababu wanajua wakichukua watalipa kodi na ku

Akizungumzia suala la hati 5,000, Lukuvi aliagiza wahusika wote kufika kuzichukua, na kwamba ifikapo mwezi Februari mwakani ambao watakuwa hawajazichukua watachukuliwa hatua.

“Kila mwananchi ambaye anaishi eneo lililopangwa na kupimwa, lazima awe na hati mkononi na kwa wale ambao hawana hati katika eneo la Mjini wafanye jitihada wawe nazo ili walipe kodi”.

Akizungumzia Watu 5,000, ambao hawajachukua hati,Mwandezi anasema, tatizo ni baadhi ya watu kuona kuwa karatasi ya Ofa ndiyo kila kitu na kutoona umuhimu wa kufuatilia hati miliki.

“Watu wakishapata Ofa wanadhani wamemaliza, na kuingia mitini, na wengine wanakuwa na mambo mengi na kufuatilia kukamilisha mchakato wa kupata hati. Waziri ameagiza tuwafuate huko huko”.

Katika ziara hiyo pa, waziri Lukuvi alibaini watendaji wa Idara ya Ardhi hawana utaratibu wa kujibu barua za wananchi wanazoandikiwa na nyingine zikiwa hazijajibiwa kwa zaidi ya miaka 18.

Kuhusu hilo Mwandezi anasema “yawezekana ni udhaifu au uzembe kwa sababu mtu kama toka 1990 hajajibiwa halafu afuatilii,japokuwa ustaarabu unatutaka tuzijibu kama ndiyo au hapana”