Lukuvi awashusha presha wenye viwanja visivyoendelezwa Dar, awapa muda zaidi

Waziri wa Ardhi William Lukuvi akizungumza kwenye mkutano 

Muktasari:

Wakazi wa Dar es Salaam walionunua viwanja katika mradi wa viwanja 20,000 jijini Dar es Salaam na kuelezwa kuwa vile visivyoendelezwa vitachukuliwa baada ya Desemba 2018 wameongezewa miezi miwili hadi Februari 2019 kuhakikisha wanaviendeleza kabla ya kuanza kwa Serikali kuvichukua visivyoendelezwa


Dar es Salaam. Unaweza kusema Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi amewatuliza walionunua viwanja katika mradi wa viwanja 20,000 jijini Dar es Salaam.

Novemba 29, 2018 Lukuvi alitangaza kiama kwa walionunua viwanja hivyo akibainisha kuwa visivyo na uzio mwisho wa kuvimiliki ni Desemba 2018 lakini leo Jumanne Desemba 18, 2018 ametamka kusogeza mbele agizo lake hilo hadi Februari 2019.

Lukuvi siku hiyo alisema baada ya mwezi Desemba viwanja vitakavyobainika kutoendelezwa Serikali itavichukua bila fidia yoyote.

Lukuvi amesogeza mbele agizo lake hilo leo katika mkutano na wakazi wa Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam kusikiliza kero na malalamiko yao kuhusu ardhi unaofanyika katika viwanja vya shule ya msingi Bunju.

Viwanja hivyo ni vile vilivyopo maeneo ya Bunju, Mpiji, Toangoma, Mwanagati, Kibada, Gezaulole Mwongozo, Mbweni na Mbweni Malindi jijini Dar es Salaam.

Amesema anatambua kuwa viwanja hivyo havijaendelezwa vikiwemo vya watendaji wa wizara  wanaojimilikisha na kuweka majina ya uongo, kwamba kwa utaratibu uliopo watabainika.

Lukuvi pia amesisitiza ni marufuku wenyeviti wa Serikali za mitaa kugonga mihuri kwenye hati za mauziano ya viwanja badala yake watumishi wa Serikali ndiyo wafanye hivyo.