Lulu: Kilikuwa kipindi kigumu chenye kila aina ya maumivu

Muktasari:

 

  • Mwigizaji Elizabeth Michael amesema kuwa kipindi cha misukosuko ya kesi yake, kilikuwa kigumu kwake na familia kilichojaa maumivu, matusi na dharau, lakini anamshukuru Mungu ameweza kuvuka salama.

Dar es Salaam. Mwigizaji Elizabeth Michael maarufu kama Lulu, amefunguka kwa mara ya kwanza tangu alipomaliza kifungo chake Jumatatu iliyopita Novemba 12, 2018, kwa kusema ilikuwa akipitia kipindi kigumu.

Lulu ametumia ukurasa wake wa mtandao wa Instagram kuelezea hisia zake baada ya kumaliza kifungo cha miaka miwili.

“Kilikuwa kipindi chenye maumivu, matusi, dharau, hukumu za wanadamu, maneno ya kulaaniwa, majina yasiyofaa na mambo mengine mengi ya aina hiyo, lakini namshukuru Mungu yote haya sikuyapokea kama yalivyokuja, bali niliyapokea kama somo/shule iliyojaa utukufu wake,” aliandika Lulu.

Lulu hakuacha kuwashukuru watu waliokuwa naye bega kwa bega kwa kipindi chote cha kesi yake mpaka kumalizika kwa kutumikia kifungo hicho.

“Kwa dhati kabisa, nichukue nafasi hii kumshukuru kila aliyeshiriki kuniombea katika kipindi kigumu sana kwangu, kwa familia yangu na watu wangu wa karibu.”

“Mliougua, mliolia na kusali pamoja nami ni wengi mno, ninaowajua na nisiowajua pia. Sala ni nyingi mno naamini imebaki hata akiba itakayoendelea kunilinda mimi na vizazi vyangu, Mungu aliyepokea sala zenu ndiye Mungu atakayewalipa,” alindika.

Lulu amekamilisha kutumikia kifungo chake cha nje na sasa yupo huru kujihusisha na maisha yake ya kawaida ambapo Mei 14, 2018 Mahakama Kuu ya Tanzania ilimuachia huru ili akatumikie kifungo cha nje.