MIAKA MITATU YA MAGUFULI: Jinsi uchumi na biashara vilivyoguswa

Muktasari:

Sh424 TRA ilisema kampuni ya Acacia inadaiwa kiasi hicho kutokana na ukwepaji wa kodi.

2016 Mwaka ambao Seri-kali ilitangaza kufunga akaunti za taasisi na mashirika ya umma katika benki binafsi.Nov.

52015; Rais Magufuli aliapishwa kuanza kui-tumikia nafasi hiyo.

Ephrahim Bahemu, Mwananchi
[email protected]

Wakati wa kampeni za kuomba kura ili achaguliwe, Rais John Magufuli ambaye ametimiza miaka mitatu tangu akalie kiti cha urais, aliahidi mambo mbalimbali ikiwamo kuendelea kuboresha mazingira ya biashara na uchumi nchini.

Baada ya kushika wadhifa huo, Magufuli amekuwa akitekeleza kwa vitendo mkakati wake wa kuwa na Tanzania iliyo bora katika sekta ya uchumi na biashara ambapo mambo mbalimbali yamefanyika ndani ya kipindi hicho.

Miongoni mwa hatua za mwanzo alizochukua kuhakikisha nchi inanufaika na rasilimali zake ili kukuza biashara na uchumi ni kupiga marufuku usafirishaji mchanga wa madini ‘makinikia’.

Machi mwaka jana, Rais Magufuli alipiga marufuku usafirishwaji wa makinikia na kutaka uchenjuaji ufanyike nchini. Hiyo ni miongoni mwa hatua zilizozua mjadala kila kona ndani na nje ya nchi.

Kutokana na hatua hiyo, makontena 277 yenye mchanga wa madini ndani yake mpaka sasa yanashikiliwa. Serikali inasema kiwango cha madini ambayo kampuni ya uchimbaji madini ya Acacia ilieleza kuwamo ndani ya mchanga huo ni tofauti na uhalisia.

Rais Magufuli aliunda kamati mbili kuchunguza usafirishaji wa mchanga na zote zilikuja na ripoti zilizoeleza kuwa taifa lilikuwa halinufaiki ipasavyo katika usafirishaji wa makinikia na mikataba ya kampuni za uchimbaji.

Katika mkakati wa Serikali kuhakikisha inapata kile ambacho ilikikosa kwa muda, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ilisema kampuni ya Acacia inadaiwa Sh424 trilioni kutokana na ukwepaji wa kodi uliofanyika tangu mwaka 2000.

Kutokana na sakata hilo Serikali ilipendekeza kufanyika kwa mabadiliko ya sheria ambayo pamoja na mambo mengine ilirejesha madini yote chini ya miliki ya nchi na kuweka vipengele vya kupitia upya mikataba ya madini.

Pia, sheria hiyo ambayo wawekezaji wengi hawakufurahishwa nayo iliweka kipengele cha ulazima wa Serikali kuwa na hisa katika kampuni ya uchimbaji madini ya aina mbalimbali.

Msamaha malimbikizo ya kodi

Mwaka 2016 kulikuwa na wimbi kubwa la biashara kufungwa, jambo hilo liliwaibua wadau wengi licha ya kuwa kufungwa na kufunguliwa kwa biashara mpya ni kawaida katika mfumo wa uchumi wa soko.

Katika mkutano wa Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) uliofanyika Machi mwaka huu, wafanyabiashara walilalamikia kuelemewa na riba na adhabu za kodi huku wakiitaja hiyo kuwa sababu mojawapo ya kufungwa kwa biashara.

Baada ya mkutano huo, Bunge kupitia kikao chake cha Bajeti lilipitisha marekebisho ya Sheria ya Usimamizi wa Kodi na kumpa mamlaka waziri mwenye dhamana kutoa msamaha wa riba na adhabu kwenye malimbikizo ya madeni ya kodi ya nyuma kwa asilimia 100.

Msamaha huo ulitoa motisha kwa wafanyabiashara kulipa madeni ya kodi zao za msingi kwa kipindi cha miezi sita, kuanzia Julai Mosi hadi Desemba 31, mwaka huu.

Msamaha huo unahusu kodi zote zinazosimamiwa na TRA ikiwamo ya mapato, maendeleo ya ufundi stadi, ongezeko la thamani (VAT), ushuru wa stempu na bidhaa, ada ya huduma za bandari na ada ya huduma ya viwanja vya ndege.

Hatua hiyo ya marekebisho ya sheria ya usimamizi wa kodi inatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha Sh500 bilioni.

Serikali kuhamishia fedha BOT

Mwanzoni mwa mwaka 2016 miezi michache baada ya Rais Magufuli kuingia madarakani Serikali yake ilitangaza kufunga akaunti za mashirika na taasisi zake kwenye benki za biashara na kuhamisha fedha zao Benki Kuu (BoT).

Taasisi za umma zilizohusika na agizo hilo ni zile za Serikali za mitaa na mihimili mitatu ya Dola, yaani Bunge, Mahakama na Serikali Kuu.

Agizo hilo pia lilitaka watendaji wakuu wote wa mashirika na taasisi za umma, kufunga akaunti zao kwenye benki za biashara na kuhamishia fedha BoT sanjari na kufungua akaunti ya mapato yao kwa aina ya fedha za mapato wanayopokea, kama ni kwa fedha za kigeni au za ndani, katika tawi la karibu la BoT mara moja.

Hatua hiyo ambayo ilikuwa kiunzi kikubwa kwa benki za biashara ilitajwa kupunguza mzunguko wa fedha katika benki hizo kiasi cha zaidi ya Sh600 bilioni.

Taarifa iliyotolewa na aliyekuwa Gavana wa BoT wakati huo ambaye sasa amestaafu, Profesa Benno Ndulu kuhusu mafanikio ya kiuchumi ya mwaka mmoja wa Serikali ya Awamu ya Tano, ilieleza kuwa uamuzi huo mbali na kuondoa fedha hizo, pia ulisaidia riba za mikopo ya benki hiyo kupungua kutoka wastani wa asilimia 15.49 hadi asilimia 13.87.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Oktoba 2016, benki nyingi za biashara zilikuwa zikitumia fedha za umma kununua dhamana za Serikali na hati fungani na kuifanya Serikali kuuziwa fedha zake, biashara ambayo imeelezwa kuwa sasa imekoma.

Marufuku ya safari za nje na mikutano hotelini

Siku chache baada ya kuapishwa Rais Magufuli alitangaza hatua zinazolenga kubana matumizi na kuimarisha mapato ya Serikali ikiwa ni pamoja na kupiga marufuku safari za nje ya nchi za maafisa wa umma.

Rais Magufuli aliagiza ziara zote za wafanyakazi wa umma nje ya nchi zipigwe marufuku mara moja na kwa yule ambaye itaonekana ni lazima asafiri sharti apate kibali kutoka Ikulu.

Alitangaza marufuku hiyo katika mkutano wake na makatibu wakuu wa wizara, manaibu wao, Gavana wa Benki Kuu na Kamishina wa TRA ikiwa ni siku tatu tu tangu aapishwe kuwa Rais.

Taarifa ya mkutano huo ilieleza kuwa Rais aliagiza majukumu yote yaliyopaswa kufanywa na maofisa wanaosafiri yashughulikiwe na mabalozi wa Tanzania walioko huko.

Kampuni za uuzaji wa tiketi za ndege ziliathirika pakubwa na mpango huo kwani watumishi wa Serikali walikuwa miongoni mwa wateja wao wakuu.

Katika mkakati huohuo wa kubana matumizi, Rais Magufuli alipiga marufuku vikao vya kikazi vya Serikali na taasisi zake kufanyika kwenye hoteli binafsi.

Agizo hilo lilisababisha hoteli nyingi nchini zilizokuwa zikiitegemea Serikali kibiashara kukabiliwa na ukata kiasi kwamba baadhi ya wamiliki wake walilazimika kubadilisha biashara.

Mikopo chechefu na kupungua kwa faida katika benki

Katika kipindi cha miaka mitatu sekta ya benki nchini ilikabiliwa na ongezeko la mikopo chechefu (NPL) ambayo pamoja na sababu nyingine pia ilichangiwa na hatua zilizochukuliwa na Serikali kudhibiti matumizi yake.

Hatua ya Serikali kuwafuta kazi watumishi wake 9,932 kwa madai ya kughushi vyeti kisha kuondolewa kwenye orodha ya mishahara kama watumishi ni miongoni mwa changamoto zilizokuwapo katika kipindi hicho na kusababisha faida katika benki kupungua.