Maagizo matano ya Serikali yaliyogonga mwamba GGM

Muktasari:

  • Yalitolewa na viongozi wa juu wa Serikali kwa nyakati tofauti yakitaka wananchi wanaoishi ndani ya leseni ya mgodi huo walipwe fidia tangu mwaka 2016

Geita. Wakati wakazi wa mitaa ya Katoma, Nyamalembo na Kompaundi wilayani Geita wanaoishi ndani ya eneo la leseni ya Mgodi wa Dhahabu  Geita (GGM), wakilazimika kusubiri siku 30 zaidi kujua hatima ya kulipwa fidia, maagizo matano yaliyotolewa kati ya 2016 na mwaka huu yameshindwa kutekelezeka.

Wananchi wanapaswa kulipwa fidia ili wahame kukimbia milipuko inayoharibu nyumba zao. Mkuu wa Mkoa wa Geita, Robert Gabriel ameunda kamati kufanya tathmini mpya ya idadi, mali na fidia wanayostahili kupatiwa ndani ya siku 30 kuanzia Novemba 12.

Kamati hiyo inayoongozwa na Mwanasheria wa Halmashauri ya Mji wa Geita, Bashiri Moja itakamilisha kazi yake Desemba 11.

Uamuzi wa kufanya tathmini upya ya nyumba zilizoko ndani ya mita 900 katika eneo la GGM aliutangaza juzi na tayari ameunda kamati ya watu 14 kutekeleza jukumu hilo.

“Februari 2016, Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST), walifanya tathmini, lakini tumebaini wao walijielekeza kuangalia nyumba zenye nyufa pekee badala ya nyumba na mali zote za wananchi wanaoathiriwa na mitetemo inayosababishwa na milipuko,” alisema Gabriel.

Kuundwa kwa kamati hiyo ni mwendelezo wa hatua na amri mbalimbali zinazotolewa na viongozi wa Serikali kuhusu suala hilo bila utekelezaji.

Septemba 26, Waziri wa Madini, Angela Kairuki aliagiza wananchi hao walipwe fidia na kuhama ndani ya siku 30 kuanzia siku hiyo. Siku 30 alizotoa waziri huyo ziliisha Oktoba 24.

Maagizo mengine ni ya Februari 23 yaliyotolewa na Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo aliyetoa siku mbili kwa GGM kukamilisha mchakato wa kuwalipa fidia wananchi.

Aliyekuwa Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Kangi Lugola (sasa Waziri wa Mambo ya Ndani) naye yumo katika orodha ya viongozi waliowahi kutoa amri zisizotekelezwa kuhusu suala hilo baada ya kutoa siku 30 kuanzia Desemba 14, 2017 kwa uongozi wa Serikali mkoani Geita kushirikiana na GGM kumaliza tatizo hilo la fidia.

Akiwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dk Merdad Kalemani (sasa Waziri wa Nishati), naye alitoa agizo Julai 2016 kwa kuipa GGM siku 30 kuwalipa fidia wananchi hao.

Akizungumzia mlolongo wa maagizo ya viongozi kuhusu suala hilo, Mkuu wa Mkoa, Gabriel alisema, “Viongozi wengi wa Serikali wametoa maagizo (wananchi) walipwe fidia, lakini mgodi haujatekeleza sasa nimeunda kamati hii itathmini madhara na itakapokamilisha GGM ilipe kwa wakati kwa mujibu wa sheria.”

Meneja Uhusiano na Mawasiliano wa GGM, Tenga Tenga aliiambia Mwananchi kwa njia ya simu kuwa hawana mpango wa kuwaondoa wananchi wanaoishi katika maeneo ambayo yako ndani ya leseni yao lakini hawayatumii katika shughuli za uchimbaji.

“GGM iko tayari kufanya majadiliano na wananchi yatakayowezesha pande hizi mbili kuishi kwa amani na bila mivutano,” alisema.

Kutokana na sintofahamu kuhusu hatima ya suala hilo, Machi 3, 2017, Mbunge wa Geita Mjini, Constantine Kanyasu aliwashauri wananchi kuchukua hatua za kisheria ili kudai haki yao ya fidia au kuendeleza maeneo yao kwa sababu mvutano kati yao na GGM haufiki mwisho.