Maazimio 15 ya EU yaibua hoja

Muktasari:

  • Baada ya bunge la EU kutoa maazimio 15 juu ya maswala mbalimbali yanayoendelea nchini,wadau mbalimbali wameuibua hoja tofauti kuhusu sakata hilo.

Dar es Salaam. Wadau wa masuala ya utawala bora kutoka makundi mbalimbali nchini, wameishauri Serikali kuepuka dosari zinazoichafua katika duru za kimataifa kupitia matukio ya ukiukwaji wa haki za binadamu, uhuru na haki ya kujieleza.

Wadau hao wamesema Tanzania ni sehemu ya dunia na kwamba Bunge la Umoja wa Ulaya (EU) linayo haki ya kutoa maoni yake kuhusu hali halisi ya mambo yanayoendelea hapa nchini.

Msingi wa kauli hiyo umechagizwa na bunge hilo kupitisha azimio lenye vipengele 15 vikihusisha masuala ya utawala wa sheria, haki za binadamu na kamatakamata ya wapinzani.

Bunge hilo la EU lilipitisha azimio namba 2018/2969 lililoandikwa Desemba 12, baada ya majadiliano yaliyofanyika mjini Brussels, Ubelgiji ikiwa ni mara ya kwanza kwa chombo cha kimataifa kutoa azimio dhidi ya Tanzania.

“Maendeleo ya aina yoyote yanakuja baada ya haki za watu wote kuheshimiwa, haki za mtu ziheshimiwe na kama tuna mila zetu wenyewe, basi kuna namna ya kuendana nazo, kwa hiyo Serikali itumie wanadiplomasia wake nje ya nchi ili kushughulikia dosari hizo,” amesema mwanasheria, Daimu Halfan.

Bunge hilo limetoa wito likitaka kuachiwa kwa wafungwa wote wa kisiasa, kufanyiwa marekebisho kwa baadhi ya sheria ikiwamo inayohusu makosa ya mitandao, sheria ya vyombo vya habari, sheria ya elektroniki na mawasiliano ya posta (Epoca) na kuachiwa watetezi wa haki za binadamu kufanya shughuli zao kwa uhuru..

Pia, limetaka tume huru itakayochunguza matukio yenye utata kama kutekwa na kukamatwa kwa waandishi wa habari na watu kutoweka katika mazingira ya kutatanisha.

Hata hivyo, Waziri wa Mambo ya Nje, Dk Augustine Mahiga aliliambia Mwananchi mwishoni mwa wiki kuwa anasubiri maelekezo ya Rais kuzungumzia suala hilo.

Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC), Onesmo ole Ngurumwa, alisema bunge la EU limetoa azimio hilo kwa sababu ni sehemu ya wadau wa maendeleo nchini na ni haki ya Taifa lolote kukemea ukiukwaji wa haki za binadamu unapojitokeza nchi nyingine.

“Kama sisi imeshindikana kusikilizwa, basi ni sahihi kupata ushirikiano wa nchi hizo. Maazimio hayo siyo kuingilia uhuru wetu ila Serikali ijitafakari kwani ni kweli uhuru na haki ya kujieleza unabanwa, wakosoaji wanakutana na hali mbaya,” alisema Ole Ngurumwa.

Aliyekuwa Mwenyekiti wa maofisa watendaji wakuu wa kampuni binafsi nchini (CEOrt), Ali Mufuruki alisema anatamani kusikia kauli ya Serikali kuhusu maazimio hayo ya bunge. “Ningependa kujua msimamo wa Serikali yetu katika suala hili, halafu ndiyo ninaweza kutoa ushauri wangu,” alisema Mufuruki.

Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Musa Salum alisema Tanzania inatakiwa kujitafakari juu ya maazimio hayo. “Tujitathmini je ni kweli yanayosemwa? Kama ni kweli basi ni suala la kurekebisha maana tumesaini mikataba ya haki za binadamu.” alisema.