Madaktari: Kila mtoto njiti anayezaliwa anapaswa kuishi

Muktasari:

Siku ya Mtoto Njiti Duniani huadhimishwa Novemba 17 kila mwaka nia ikiwa ni kuhamasisha huduma bora ili kuokoa uhai wa watoto hao kutokana na takwimu kuonyesha vifo vingi vya watoto wachanga ni njiti.

Dar es Salaam. Madaktari bingwa na wauguzi wa watoto nchini wameamua kuadhimisha Siku ya Mtoto Njiti Duniani kwa kurusha maputo juu kuonyesha kila mtoto anayezaliwa anapaswa kuwa hai.

Mkuu wa Idara ya Watoto katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Dk Mary Charles amesema haikubaliki kuona baadhi ya watoto wanapoteza maisha kwa sababu wamezaliwa njiti.

Akizungumza leo wakati wa maadhimisho hayo, Dk Mary alisema takwimu zinaonyesha  vifo vya watoto wachanga njiti ni karibu theluthi ya vifo vyote vya watoto chini ya miaka mitano.

"Kwa kiwango kikubwa watoto wachanga wanaofariki ni njiti, hali hii haikubaliki lazima tufanye juhudi za kuhakikisha kila mtoto anayezaliwa katika mikono yetu anakwenda nyumbani kwao akiwa hai," alisema Dk Mary.

Alisema MNH imefanikiwa kukarabati jengo la watoto wachanga ikiwa ni moja ya mikakati ya kuboresha huduma.

"Tumedhamiria kuwaendeleza kielimu watumishi wetu ili tuendelee kuboresha huduma kwa watoto wachanga na tutaanza rasmi mwakani 2019," alisema.

Rais wa Chama cha Madaktari Bingwa wa Watoto, Dk Sekela Mwakyusa alisema upatikanaji wa vifaa maalum na huduma bora kutasaidia kuokoa uhai wa kila mtoto anayezaliwa.