Magufuli aanika mchongo wa wanaodaiwa kuiba dhahabu

Muktasari:

  • Rais Magufuli aelezea kwa kina sakata la dhahabu iliyokamatwa Mwanza ikitaka kutoroshwa, ampongeza IGP kwa kuwezesha kukamatwa kwa wahusika na askari waliotaka kuhongwa fedha ili wawaachie wahalifu

Dar es Salaam. Rais John Magufuli amelipongeza Jeshi la Polisi na Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Simon Sirro kwa kufanikishwa kukamatwa kwa dhahabu iliyokuwa inasafirishwa kwenda nje ya nchi.

Akizungumza leo Jumatano Januari 9, 2019 wakati wa hafla ya kuwaapisha viongozi kadhaa aliowateua jana akiwemo waziri wa madini, Rais Magufuli amesema uimara wa kiongozi huyo ndio umefanikishwa kukamatwa kwa watuhumiwa hao na askari waliotaka kufanikisha utoroshaji huo.

Amesema anazo taarifa za kutosha kuwa askari waliowakamata wahalifu hao walikula njama na kutaka kuwasaidia kutoroka baada ya kuahidiwa Sh1 bilioni.

“Mie ninashangaa watu wanaongea vitu wasivyovijua, nina taarifa za kutosha na katika hili nimpongeze sana IGP alisimama kidete kuhakikisha wote wanakamatwa na dhahabu ile inapatikana,” amesema.

“Inauma unapoona kilo zaidi ya 300 zenye thamani ya zaidi ya Sh30 bilioni zinakamatwa zikisafirishwa. Wameshaiona Tanzania ni nchi ambayo unaweza kufanya lolote,” ameongeza.

Akizungumzia mchongo mzima ulivyokuwa, Rais Magufuli amesema anazo taarifa za kutosha kuwa askari waliodai kuwafuatilia wahalifu hao nao walikuwa sehemu ya uhalifu

“Watuhumiwa walikamatwa tarehe 4 Misungwi (Mwanza), wakarudishwa mjini na kikosi cha polisi kilichoongozwa na Superintendent.”

“Walipoona wamewashika na mali ile wakawapeleka kituo cha polisi lakini hawakuwaingiza ndani wakakaa kwenye gari wakawa wanafanya majadiliano jinsi ya kuwahonga,” amesema.

Ameongeza, “Askari waliahidiwa Sh1 bilioni na wakapewa Sh700 milioni. Wakaondoka nao hadi kwenye Kivuko Kamanga wakawa wanawasindikiza wale wahalifu kwenda Sengerema kwa ajili ya kuwapatia milioni 300 iliyosalia.”

Amesema kundi hilo likiwa njia taarifa zikamfikia Kamanda wa Polisi Mkoa na mawasiliano yakafanyika hadi kumfikia yeye aliyeagiza wakamatwe.

Rais Magufuli amesema walipofika mbele walikuta kizuizi cha polisi wakasimamishwa ndipo gari la polisi lililokuwa nyuma likapiga king’ora na kudai walikuwa wakiwafuatilia.

Amesema aliagiza polisi hao wakamatwe na kunyang’anywa silaha kisha wakafungwa pingu na kurudishwa Mwanza ambapo watapelekwa mahakama ya kijeshi kisha baadaye mahakama za kiraia.