Magufuli afuta maelekezo mapya matumizi ya bendera, nembo na wimbo wa Taifa

Muktasari:

Wakati wananchi wakihoji kuhusu maelekezo mapya ya matumizi ya bendera, nembo na wimbo wa Taifa, Rais John Magufuli amefuta maelekezo hayo mapya akisema kama kuna mabadiliko basi lazima yafanyike kwa kuzingatia taratibu zote kwa kuwa jambo hilo ni la kitaifa, sio la mtu mmoja


Dar es Salaam. Rais John Magufuli amefuta barua ya Wizara ya Elimu kwenda kwa vyuo mbalimbali nchini Tanzania inayoeleza matumizi sahihi ya bendera, nembo na wimbo wa Taifa.

Leo Ijumaa Desemba 14, 2018 katika taarifa ya Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Gerson Msigwa inaeleza kuwa Rais Magufuli amefuta barua hiyo.

Katika barua hiyo yenye kumbukumbu namba CHA 56/193/02/16 ya Novemba 23, 2018 iliyoandikwa na Wizara ya Elimu  kwenda kwa wakuu wa vyuo vya ualimu, vyuo vya ufundi na maendeleo ya jamii, vyuo vikuu na vishiriki na taasisi zilizo chini ya wizara hiyo  inaeleza imepokea maelekezo kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani kuhusu matumizi sahihi ya rangi ya bendera na wimbo wa Taifa.

“Rais amesema barua hiyo yenye kichwa cha habari ‘Matumizi Sahihi ya Bendera, Nembo na Wimbo wa Taifa’, imetoa maelekezo ambayo yanaathiri uzalendo wa Watanzania na inaleta mkanganyiko wa tafsiri ya rangi na alama zilizomo katika bendera ya Taifa,” inaeleza taarifa hiyo ikimnukuu Rais Magufuli.

“Hata mimi mwenyewe tangu nasoma shule hadi leo nafahamu kuwa bendera ya Taifa ina rangi ya njano  na sio rangi ya dhahabu, na rangi hiyo ya njano inawakilisha madini yote, sio dhahabu peke yake.”

Katika taarifa Rais Magufuli anasema, “Kwa hiyo nimeamua kuifuta barua hiyo na kama kuna mabadiliko basi lazima yafanyike kwa kuzingatia taratibu zote kwa kuwa jambo hili la kitaifa, sio la mtu mmoja.”

Inaeleza kuwa Rais ameagiza bendera, nembo na wimbo wa Taifa viendelee kutumika kama ilivyokuwa kabla ya kuandikwa kwa barua hiyo na ametoa wito kwa Watanzania kuendelea kuwa wazalendo, kuipenda nchi yao na kuitangaza popote walipo ilimradi wanazingatia maslahi ya Taifa.

 Inavyoeleza barua hiyo

 “Kutokana na makosa hayo Wizara ya Mambo ya Ndani inaelekeza kuwa wimbo wa Taifa utapigwa kwenye dhifa za kitaifa, endapo hadhi ya sherehe haitambuliki, taasisi italazimika kuomba kibali kwa waziri mwenye dhamana,” inaeleza barua hiyo.

“Wimbo unatakiwa kuimbwa kwa ukamilifu beti zote mbili kwa kuzingatia nota na maneno.”

Pia ilizungumzia rangi za Bendera ya Taifa.

“Rangi za Bendera ya Taifa ni kijani, dhahabu, nyeusi na bluu. Ni makosa kutumia rangi ya njano na uwiano wa bendera ni 2/3 katika urefu na upana.”