Magufuli atuma salamu za rambirambi kifo cha makamu mkuu wa Udom

Muktasari:

  • Rais John Magufuli ametuma salamu za rambirambi  kwa mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Benjamin Mkapa kufuatia kifo cha Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa Egid Mubofu

Dar es Salaam. Rais John Magufuli ametuma salamu za rambirambi  kwa mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Benjamin Mkapa kufuatia kifo cha Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa Egid Mubofu.

Profesa Mubofu amefariki dunia leo Jumanne Desemba 18, 2018 Pretoria, Afrika Kusini alikopelekwa kwa ajili ya matibabu zaidi akitokea taasisi ya tiba ya mifupa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (Moi) alikokuwa akipatiwa matibabu ya kiharusi.

Taarifa iliyotolewa leo na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Gerson Msigwa inasema Rais Magufuli amemuomba Mkapa kufikisha salamu zake za pole kwa familia ya marehemu, wahadhiri, wanafunzi na wafanyakazi wa Udom na kwenye  jumuiya na taasisi zote ambazo marehemu alifanya kazi.

“Nimesikitishwa  sana na kifo cha Profesa Mubofu, nitamkumbuka kwa uchapakazi wake, ubinifu, uadilifu na uaminifu mkubwa aliouonesha katika utumishi wake kwa Taifa ikiwemo kazi nzuri aliyoifanya katika Shirika la Viwango la Taifa (TBS) akiwa mkurugenzi mkuu kabla ya kuteuliwa kuwa makamu mkuu wa Udom,” amesema Rais Magufuli.