Mahakama yamuonya MC Luvanda

Muktasari:

  • Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam, leo Jumatatu imemuonya mshereheshaji maarufu nchini Tanzania, Anthony Luvanda maarufu kama MC Luvanda kuhakikisha anazingatia masharti ya dhamana

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imemuonya mshereheshaji maarufu nchini Tanzania, Anthony Luvanda maarufu kama MC Luvanda kwa kusafiri bila ya ruhusa ya Mahakama.

Onyo hilo limetolewa leo Jumatatu Novemba 19, 2018 na Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi mbele ya mshtakiwa Luvanda, wakili wake Jebra Kambole na wakili wa Serikali Mwandamizi, Kishenyi Mutalemwa.

Hatua hiyo ilifikiwa baada ya wakili Kishenyi kuieleza Mahakama kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na kwamba mara ya mwisho kulikuwepo na amri ya Mahakama ya kumkamata mshtakiwa huyo kwa kusafiri bila ruhusa ya Mahakama.

Wakili Kishenyi ameeleza Mahakama kwa sababu ametokea akumbushwe masharti ya dhamana.

Baada ya wakili Kishenyi kueleza hayo, wakili wa Luvanda, Jebra Kambole amedai yeye hana pingamizi kuhusu mshtakiwa kukumbushwa masharti ya dhamana na akaomba radhi kwa yaliyotokea na kwamba mambo hayo hayatajirudia tena.

Hakimu Shaidi alimwambia mshtakiwa huyo kila kitu kina nidhamu yake, pia hata katika kesi na kufika mahakamani kuna nidhamu yake.

Kitendo cha wewe kusafiri bila kuitaarifu Mahakama si kitu kizuri, ukitaka kusafiri toa taarifa.

Hakimu Shaidi ameiahirisha kesi hiyo hadi Desemba 18, 2018 na akamuonya mshtakiwa huyo afuate utaratibu.

Awali, Hakimu Shaidi Oktoba 23, mwaka huu akitoa  hati ya kukamatwa kwa Luvanda wakati kesi hiyo ilipopangwa kwa ajili ya kutajwa lakini mshtakiwa huyo hakuwepo mahakamani.

MC Luvanda pamoja na kampuni yake, wanakabiliwa na mashtaka matatu likiwemo la kutumia kikoa ambacho akijasajiliwa Tanzania.

Luvanda anashtakiwa pia kwa kutoa maudhui mtandaoni bila ya kuwa na kibali cha Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).

 

 

 

 

 

 

 

Mbali na luvanda mshtakiwa mwingine katika kesi hiyo ni kampuni ya Luvanda ya Home of Company Limited.

MC Luvanda  na kampuni anayomiliki ya Home of Company Limited  wanadaiwa kutumia kikoa ambacho akijasajiliwa Tanzania.

Inadaiwa kuwa  kati ya Februari 24 na Septemba 2018 katika jiji la Dar es Salaam,  mshtakiwa huyo alianzisha na kutumia mtandao wa  www.mcluvanda.com ambao haukuwa na kikoa cha .tz.

Pia inadaiwa kuwa  katika kipindi hicho mshtakiwa alianzisha na kutumia mtandao huo ambao haukuwa na kikoa cha .tz.

Aidha imedaiwa,mshtakiwa huyo alitoa Huduma ya online bila ya kuwa na kibali.

Mc Luvanda anadaiwa kuwa katika kipindi hicho  alitoa huduma hiyo kupitia online TV  ifahamikayo kama MC Luvanda pasipokuwa na kibali toka TCRA.

Baada ya kusomewa mashtaka hayo Mshtakiwa Luvanda alikana mashtaka hayo na yuko nje kwa dhamana baada ya kutimiza masharti ya dhamana ya kuwa na mdhamini mmoja Mwenye barua na kitambulisho ambaye alisaini bondi ya Sh 5 milioni.