Mahakama yataka uchunguzi kesi ya kina Kitilya ukamilike

Muktasari:

Kesi inayomkabili aliyekuwa Mwenyekiti wa Kampuni inayoshughulikia Uwekezaji wa Mitaji na Dhamana (Egma), Harry Kitilya na maofisa wa benki ya Stanbic, Shose Sinare na Sioi Solomon imeahirishwa hadi Novemba 30, 2018

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeutaka upande wa mashtaka kufanya jitihada kukamilisha upelelezi katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili, aliyekuwa Mwenyekiti wa Kampuni inayoshughulikia Uwekezaji wa Mitaji na Dhamana (Egma), Harry Kitilya na wenzake wawili.

Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi leo Jumatatu Novemba 19, 2018 ameutaka upande wa mashtaka kufanya jitihada za kukamilisha upelelezi wa kesi hiyo ili hatma ya washtakiwa hao ijulikane.

Ni baada ya Wakili wa Serikali Mwandamizi, Mutalemwa Kishenyi kueleza kesi ilipangwa kwa ajili ya kutajwa na upelelezi wake bado haujakamilika na kwamba wanaelekea ukingoni kukamilisha.

Baada ya Wakili Kishenyi kueleza hayo, wakili wa utetezi Alex Mgongolwa amehoji ni ukingo gani huo ambao unazungumziwa na upande wa mashtaka.

Wakili Kishenyi ameongeza kudai upelelezi wa kesi hiyo, kimsingi upo katika hatua nzuri na akaomba ipangiwe tarehe nyingine ya kutajwa.

Baada ya kusikiliza hoja hizo, Hakimu Shaidi ameiahirisha kesi hiyo hadi Novemba 30, mwaka huu na kuutaka upande wa mashtaka kufanya jitihada kukamilisha upelelezi.

Mbali na Kitilya ambaye pia aliwahi kuwa Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni waliokuwa maofisa wa benki ya Stanbic,  Shose Sinare na Sioi Solomon.

Washitakiwa hao kwa pamoja wanakabiliwa na mashitaka ya kula njama, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na kutakatisha fedha.

Wanadaiwa kutenda makosa hayo kati ya Machi 2013 na Septemba 2015 wakati wa mchakato wa mkopo wa dola za Marekani milioni 550 kwa Serikali ya Tanzania kutoka Benki ya Standard Uingereza.

Wanadaiwa kuwa Machi 2013 jijini Dar es Salaam walijipatia Dola za Marekani milioni sita, wakionyesha kuwa fedha hizo zilikuwa ni malipo ya ada ya uwezeshaji upatikanaji wa mkopo na zililipwa kupitia Kampuni ya Egma T Ltd.

Washitakiwa hao wanadaiwa kutakatisha fedha kwa kuhamisha, kuchukua na kuweka kiasi cha Dola za Marekani milioni sita katika akaunti tofauti tofauti za benki.

Kati ya  Machi 2013 na Septemba 2015, wanadaiwa kuwa waliweka pesa hizo katika akaunti mbalimbali zilizomilikiwa na kampuni ya Egma na kwamba walipaswa kufahamu kuwa pesa hizo ni mazao ya uhalifu wa kughushi.