Mahakama yatupa kesi mwili ukifikisha siku 161

Muktasari:

  • Mahakama Kuu Mbeya imeitupa na kufuta rufaa ya kesi iliyofunguliwa na ndugu wa marehemu Frank Kapange (21) dhidi ya Jeshi la Polisi ya kuiomba itengue uamuzi uliotolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoani hapa.

Mbeya. Mahakama Kuu Mbeya imeitupa na kufuta rufaa ya kesi iliyofunguliwa na ndugu wa marehemu Frank Kapange (21) dhidi ya Jeshi la Polisi ya kuiomba itengue uamuzi uliotolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoani hapa.

Mahakama ya Hakimu Mkazi ilikuwa imetupilia mbali maombi ya ndugu hao na kuamuru marehemu azikwe.

Frank (pichani) alifariki Juni 4, kifo chake kikigubikwa na utata kutokana na mazingira yake baada ya ndugu kudai alifariki dunia kwa kipigo akiwa mikononi mwa polisi.

Ndugu waligoma kuuchukua mwili huo na hadi jana saa 12 jioni ulikuwa umefikisha siku 161 ukiwa mochwari ya Hospitali ya Rufaa Mbeya.

Agosti 24, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa mahakama hiyo, Michael Mteite aliamuru mwili wa Frank kuchukuliwa na ndugu ili wakauzike baada ya kutupilia mbali maombi ya familia ya kuiomba mahakama hiyo iamuru kufanyika kwa uchunguzi wa kiini cha kifo chake.

Ndugu hao walidai kutoridhika na uamuzi huo hivyo wakaamua kukata rufaa Mahakama Kuu ambayo jana ilitoa uamuzi wa kuifuta kesi hiyo baada ya kujiridhisha kwamba mlalamikaji hakufuata taratibu zilizopaswa wakati wa kufungua kesi hiyo.

Akitoa uamuzi huo, Jaji Paul Ngwembe alisema mahakama yake ilisikiliza na kuzipitia hoja za pande mbili na kujiridhisha kwamba hoja zilizowasilishwa na Wakili upande wa utetezi hazina mashiko na utaratibu mzima uliotumika kufungua kesi hiyo haukuwa sahihi.

Jaji Ngwembe alisema kabla ya kufungwa kesi hiyo mahakamani walipaswa kuwa na ripoti ya kitaalamu inayoonyesha mwili wa Frank ulifanyiwa uchunguzi ambao ungetoa mwelekeo wa kifo chake.

“Lazima kuwe na ripoti ya kitaalamu kuhusiana na kifo chake ndipo walalamikaje wafungue kesi kulingana na ripoti itakayoonyesha marehemu alikufa kwa sababu ipi na hapo ndipo walalamikaji wangekuja na mtuhumiwa wanaodai alihusika,” alisema Jaji Ngwembe.

Jaji Ngwembe alisema hoja iliyowasilishwa na wakili wa utetezi, Moris Mwamwenda kwamba kukosewa kwa hati ya kiapo ambacho kilisainiwa na wakili badala ya mlalamikaji kusingefanya kufutwa kwa kesi ya msingi na badala yake hakimu angeiondoa kesi hiyo ili waweze kurekebisha na kuirudisha mahakamani, haina mashiko kwani hilo ni takwa la kisheria hivyo mawakili wa Jamhuri walikuwa sahihi.

Alisema, “hati ya kiapo inaonyesha imesainiwa na mtu asiyehusika badala ya mlalamikaji, lakini maelezo yaliyopo katika kiapo hicho ni ya mlalamikaji, hivyo hili lipo kisheria kabisa ilipaswa isainiwe na mhusika (mlalamikaji) na kionyeshe kilipotolewa’.

Alisema suala la Mahakama ya Hakimu Mkazi kutoa uamuzi kwa kusikiliza upande mmoja wa Jamhuri ulikuwa sahihi kutokana na wakili wa utetezi kushindwa kupeleka utetezi ndani ya muda uliopangwa bila kutoa sababu zozote.

Baada ya kusoma maelezo ya hukumu hiyo, Jaji Ngwembe alisema anaifuta kesi hiyo na kama ndugu wanahitaji kuendelea nayo ni lazima waanze upya kufuata taratibu zinazotakiwa ikiwamo kufanya uchunguzi wa kitaalamu wa kijana wao na ripoti yao ndio itakayowasilishwa mahakamani.

Uamuzi huo uliwachanganya ndugu wa marehemu huyo kutokana na mtihani waliopewa huku wakibainisha kwamba hawajaridhika na hukumu hiyo.

Nje ya mahakama hiyo, msemaji wa familia hiyo, Julius Kapange alisema ‘Daaa! Hii imetuchanganya zaidi, uamuzi uliotolewa hatujaridhika nao kabisa, lakini ni hatua gani tutachukua baada ya hili… tunamsubiri wakili wetu atatuambia nini, hapo ndio tutatoa uamuzi wetu mwingine’.