Maiti iliyokuwa ikigombewa Moshi kuzikwa leo

Muktasari:

  • Ni baada ya hukumu kutolewa juzi na upande wa ndugu wa marehemu kuibuka washindi dhidi ya mumewe ambaye alifungua kesi akitaka kumzika mkewe kwa imani ya Kiislamu

Moshi. Baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi kutupilia mbali maombi madogo ya kumzika Betty Aseri Kileo yaliyofikishwa mahakamani hapo na Zuberi Shango aliyedai kuwa ni mume wa marehemu, familia imepanga kufanya mazishi hayo leo.

Akizungumza na Mwananchi Digital jana, Halima Hussein, ambaye ni dada wa marehemu alisema familia imeridhika na uamuzi wa mahakama na jana ilikuwa ikiandaa mipango ya maziko, lakini hakusema watazikia eneo gani.

“Tunazika kesho (leo), wapi tunakwenda kuzika itajulikana baadaye,” alisema Halima.

Awali, Shango alipeleka maombi namba 24 ya 2018 katika mahakama hiyo chini ya mawakili wake Mussa Mziray, Elia Kiwia, Wilhad Kitaly na Tumaini Materu.

Katika maombi yake aliomba kibali cha kumzika Fatuma Kileo, ambaye alidai kuwa ni mke wake akidai kwamba alifunga naye ndoa mwaka 2005. Alidai marehemu ambaye awali alikuwa akiitwa Betty Kileo, alibadilisha jina baada ya kufunga naye ndoa na kuitwa Fatuma Kileo na kuwa mwislamu.

Wakati waleta maombi wakieleza hayo, wajibu maombi walipinga madai hayo na kueleza kuwa Betty hakuwahi kubadilisha jina na kwamba bado alikuwa ni mkristo.

Wajibu maombi ambao walipewa haki ya kumzika marehemu, walikuwa wakitetewa na Wakili Godwin Sandi. Akitoa uamuzi wa maombi hayo juzi, Hakimu Bernazitha Maziku alisema mahakama imeona maombi hayo hayana mashiko na hivyo imeyatupilia mbali na kutoa haki ya kuzika kwa wajibu maombi.

Maziku alisema mahakama hiyo katika kutoa uamuzi ilijikita katika maswali matatu ambayo ni kama kulikuwa na ndoa kati ya Fatuma na mleta maombi, kama Fatuma na Betty ni mtu mmoja na iwapo kulikuwa na mabadiliko ya majina baada ya ndoa kama ilivyoelezwa mahakamani hapo.

Alisema awali katika maelezo ya mawakili wa pande zote mbili, hakuna aliyepinga kwamba kulikuwa na ndoa ya Shango na Fatuma Kileo, na hakuna ubishi kuwa ndoa hiyo ilidumu kwa miaka 13. Maziku alisema jambo ambalo lilikuwa kwenye ubishi ni kama Fatuma na Bety ni mtu mmoja na kama kulikuwa ubadilishaji wa majina baada ya ndoa kufungwa.

“Ushahidi uliopo kwa pande zote ambao pia upo kwenye kiapo cha waleta maombi, pande zote zinakubali marehemu alikuwa akiitwa Betty na ndiyo majina aliyorithi kutoka kwa wazazi wake na hakuna ubishi kuwa ndilo jina lake la utotoni na  ndilo alilokuwa nalo ” alisema.

Hakimu alifafanua kuwa, “kama alikuwa mfuasi wa dini ya kikristo na alibadili jina baada ya ndoa, kulikuwa na haja ya mleta maombi kuleta cheti cha ndoa chenye jina la Betty Aseri Kileo, jina ambalo alikuwa akilitumia.”

“Au alipaswa kuleta nyaraka za marehemu kubadilisha jina la Betty aliloliacha na kupewa la Fatuma, uhitaji wa kusajili nyaraka ulikuwa ni pamoja na nyaraka za kubadili jina.”

Hakimu alisema, “Hivyo maombi haya mahakama imeona hayana mashiko na yametupiliwa mbali, haki ya kuzika imerudi kwa wajibu maombi na ambaye hajaridhika anaweza kukata rufaa.”

Kesi hiyo ilifunguliwa katika mahakama hiyo Oktoba 26, siku moja baada ya Betty kufariki dunia akiwa nyumbani kwake Himo, kwa mujibu wa ndugu zake.