Majaliwa asema Rais hapendi watu walipe nauli kufuata huduma za afya

Muktasari:

  • Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ametembelea kituo cha afya cha Nkowe na kukagua ujenzi wa gereza la Wilaya ya Ruangwa pamoja na mradi wa ujenzi wa nyumba za makazi ya askari Magereza wa gereza hilo. Katika ziara hiyo amewaasa wananchi kutumia kituo hicho cha afya na kukitunza.

Dar es Salaam. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ametembelea kituo cha afya cha Nkowe na kukagua ujenzi wa gereza la Wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi pamoja na mradi wa ujenzi wa nyumba za makazi ya askari magereza wa gereza hilo.

Waziri Mkuu ametembelea miradi hiyo leo Jumapili, Novemba 18, 2018 akiwa katika ziara yake ya kikazi Wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi ambapo amewataka wananchi kulinda kituo hicho cha afya.

Amesema kwa sasa wananchi hao hawana sababu ya kulipa nauli kwenda Ruangwa kufuata huduma za vipimo na matibabu katika hospitali ya wilaya kwani baadhi yake kama upasuaji, maabara, mama na mtoto zinapatikana katika kituo hicho.

“Rais John Magufuli anataka kila Mtanzania apate huduma za afya karibu na makazi yake ili asilipe nauli au kutembea umbali mrefu kufuata huduma za afya,” amesema Majaliwa.

Mganga Mfawidhi wa kituo hicho, Dk Paul Mbinga amesema kituo hicho kinahudumia  wakazi 5,264 wa Kata ya Nkowe, Chienjele, Nandagala, Likunja na Mnacho.

Dk Mbinga amesema mradi wa ujenzi wa kituo hicho cha afya uliogharimu Sh500 milioni, umepunguza gharama kama kwenda kutibiwa katika hospitali ya wilaya ambayo ipo umbali wa kilomita 20. “Mradi huu umeimarisha mifumo ya huduma kwa watoto, wazee, watu wenye ulemavu na vijana”.