Majaliwa ashuhudia wizi, uharibifu mradi NSSF Dar

Muktasari:

  • Ni baada ya kuutembelea na kukuta baadhi ya vitu vimenyofolewa, aagiza pande mbili zinazohusika kuanza kuulinda kuanzia sasa

Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesikitishwa na uharibifu wa mali na wizi unaoendelea kwenye eneo la mradi wa nyumba unaojengwa kwa ubia kati ya Shirika la Hifadhi ya Jamii la Taifa (NSSF) na Kampuni ya Azimio Housing Estate katika eneo la Dege Beach, Kigamboni jijini Dar es Salaam.

Majaliwa amewaagiza Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, William Erio na Mkurugenzi Mkuu wa Azimio Housing Estate Limited (AHEL), Mohammed Iqbal wakutane na Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Charles Kichere kujadiliana namna ya kudhibiti wizi.

Taarifa iliyotolewa jana na Ofisi ya Waziri Mkuu ilisema Majaliwa alitembelea eneo hilo jioni na baada ya kufika zinapojengwa nyumba zaidi ya 7,000 alionyesha kusikitishwa na uharibifu wa mali pamoja na wizi unaofanyika sehemu hiyo.

“Kuna mpango gani wa ulinzi wa mali hapa, mali zinaendelea kuibiwa, tutakuja kuanza ujenzi hapa na kukuta hakuna mali hata moja. Ulinzi lazima uimarishwe, pande zote mbili za mradi huu eneo la ujenzi na eneo la kuhifadhia vifaa vya ujenzi,” alisema.

Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Erio alimwahidi Waziri Mkuu  kuwa watatekeleza maagizo yake na kujadiliana namna ya kuimarisha ulinzi pamoja na kutatua changamoto ya wizi wa mali unaoendelea katika eneo hilo.

Mkataba kati ya NSSF na Azimio Housing Estate Limited ulisainiwa mwaka 2012 na kuanzisha kampuni ya Hifadhi Builders na AHEL ina asilimia 55 huku NSSF ikiwa nazo 45.

Katika asilimia 55 za AHEL, 20 ni ardhi iliyotoa kwa ajili ya mradi na 35 inatakiwa kuweka fedha taslimu.

Mradi huo unahusisha ujenzi wa nyumba 7,460 na jumla ya gharama za mradi zilikadiriwa kuwa Dola 653,436,675 za Marekani ambazo kati yake ujenzi ungegharimu Dola 544,530,562 za Marekani wakati gharama za ardhi zingekuwa Dola 108,906,113.

Kwa fedha za Tanzania mradi pamoja na ardhi ungegharimu Sh1.5 trilioni.

Hadi kufikia Juni, 2018 NSSF walishailipa Hifadhi Builders Dola 133,838,662.2 (sawa na Sh305.8 bilioni) kama mchango wake kwenye ujenzi wa mradi huo wakati kampuni ya Azimio ikitoa Dola 5,500,000 (sawa na Sh12.6 bilioni).