Majaliwa kuzindua michezo vyuo vikuu, wanafunzi 4,000 kushiriki

Muktasari:

  • umatatu Desemba 17, 2018 Waziri Mkuu Kassim Majaliwa atazindua michezo ya Vyuo Vikuu vya Afrika Mashariki itakayowahusisha wanafunzi 4,000

Dodoma. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kesho atakuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa michezo ya Vyuo Vikuu vya Afrika Mashariki itakayofanyika Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) na kuwakutanisha wanafunzi 4,000.

Akizungumza leo Jumapili Desemba 16,  2018 ofisa uhusiano wa Udom,  Beatrice Mtenga amesema michezo hiyo itaanza kesho hadi Desemba 21, 2018.

Kaimu Makamu Mkuu wa Udom,  Profesa Peter Msoffe amesema maandalizi muhimu yamekamilika ikiwa ni pamoja na viwanja kuwa katika hali nzuri.

"Michezo hii itashirikisha vyuo 50 kutoka nchi za Afrika Mashariki na tayari maandalizi yamekamilika. Viwanja na mabweni yako katika kiwango kizuri," amesema.

Mmoja wa wasimamizi wa michezo hiyo, Wiston Mdegela amesema itawashirikisha wanafunzi 4,000.

Amesema michezo 19 itachezwa katika viwanja vya chuo hicho na kuwataka wakazi wa Dodoma na mikoa mingine kufika ili kujionea vipaji  vya wanafunzi.