Makamba: Tunahitaji ‘udikteta’

Saturday October 11 2014

Mbunge wa Jimbo la Bumbuli na Naibu Waziri wa

Mbunge wa Jimbo la Bumbuli na Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba (kushoto), akizungumza na waandishi wa gazeti hili, Ibrahim Yamola na Fidelis Butahe (kulia), Dar es Salaam jana. Picha na Venance Nestory      

By Fidelis Butahe na Ibrahim Yamola, Mwananchi

Dar es Salaam. Iko dhana kuwa ili Tanzania ipige hatua kimaendeleo inahitaji kiongozi anayethubutu kufanya uamuzi mgumu hasa kuwawajibisha viongozi wabadhirifu na wazembe, lakini Mbunge wa Bumbuli (CCM), January Makamba amekwenda mbali zaidi; anasema dawa ni kufanya uamuzi wa kidikteta.

Makamba alitoa kauli hiyo jana katika mahojiano maalumu na Mwananchi Jumamosi, ofisini kwake jijini Dar es Salaam.

Mbunge huyo ambaye hivi karibuni alitangaza nia ya kugombea urais katika Uchaguzi Mkuu mwaka 2015, ametoa kauli hiyo wakati nchi ikijiandaa kwa uchaguzi huo huku tayari watu mbalimbali, hasa kutoka chama tawala cha CCM wakiwa wameshaanza kujinadi.

“Moja ya vitu vitakavyozuia rushwa ni adhabu kali ambayo itaonekana. Kwa nini madikteta wanawaua watu hadharani? Wanachojaribu kukionyesha ni kwamba kama siku moja mtu akijaribu kuwapindua atapelekwa uwanjani na kupigwa risasi hadharani. Lengo ni kuwatia watu hofu,” alisema.

Alisema, “Moja ya namna ya kupambana na rushwa ni kuwatia watu hofu, kwamba ukikamatwa yatakayokukuta ni kama yanayowakuta wenzako.”

Alisema ili kupambana na rushwa ni lazima kuwekwe mbinu za kivita na kwamba kama hilo lisipofanyika ni sawa na kupoteza muda.

“Serikali itakuwa inakusanya mapato na kupanga mambo yake, lakini asilimia 50 ya mambo hayo yanarudi mikononi mwa watu,” alisema.

Makamba alisema mmomonyoko wa maadili ni moja ya sababu inayofanya nchi ichelewe kupata maendeleo.

“Kuna wizi na ubadhilifu mkubwa siyo tu kwa viongozi wa kisiasa, hasa kwa watendaji na watumishi wa kada za kati na chini. Watu wanawatizama wabunge na waziri pekee wakati wapo wahasibu wa wizara na halmashauri,” alisema.

Maadili

Alisema suala la maadili lipo katika sura mbili, ya kwanza ikiwa ni adhabu za kijamii na pili ni adhabu za kisheria.

“Katika adhabu za kijamii, ni lazima kujengeke utamaduni kwenye jamii wa kuwatenga, kuwachukia watu ambao wanapata kipato kisicho halali. Katika adhabu za kisheria, cha kufanya ni kuanzisha mahakama maalumu na kubadilisha sheria na kuyaweka kwa pamoja makosa ya rushwa na ubadhirifu kama makosa ya uhujumu uchumi,” alisema.

Mbunge huyo kijana alisema kwamba kitendo cha daraja linalotakiwa kujengwa kwa Sh800 milioni, lakini likajengwa kwa Sh200 milioni ni sawa na uhujumu uchumi na kusisitiza kuwa lazima adhabu ziongezeke.

“Kuna udhaifu wa kitaasisi katika kuchunguza na kuhukumu makosa ya rushwa. Kesi zinakaa miaka mingi bila kuisha na kumbuka kuwa wenye makosa hayo wana fedha na uwezo wa kutafuta mawakili wazuri, “ alisema, Aliongeza,

 “Tunatakiwa kuweka tafsiri mpya ya nini hasa maana ya uhujumu uchumi na kuyapandisha daraja makosa hayo ili watakaobainika wafungwe miaka 30 jela au kufungwa maisha. Hizi taasisi za kuchunguza na kuhukumu makosa ya rushwa tunatakiwa kuzipanga upya.”

Alisema jambo jingine ni kuwa na mahakama maalumu za kusikiliza na kutoa uamuzi wa kesi za uhujumu uchumi.

“Kama mfumo wa uchaguzi unaingiza viongozi kwa rushwa au viongozi waliowahi kula rushwa, tusahau kabisa nchi hii kuondokana na rushwa. Hapo ni pa kupafanyia kazi sana,” alisisitiza.

Alisema licha ya kuwa nchi ina Sheria ya Matumzi ya Fedha za Uchaguzi, lakini imekosa usimamizi na kufafanua kwamba ni vyema sasa kuwa na taasisi mahususi kwa ajili ya usimamizi na ufuatiliaji wa sheria hiyo.

“Kingine ni ujasiri wa kuwafuta uongozi na kuwapiga marufuku wagombea wanaogawa fedha ili kupata madaraka,” alisema.

Urais uchaguzi 2015

Akizungumzia nafasi yake ya kuwa rais wa Tanzania na mchakato wa CCM katika kuteua jina moja la mtu anayefaa kugombea urais kwa tiketi ya chama hicho alisema, “ Taasisi ya kujipanga ni CCM ambayo ndiyo yenye dhamana ya kuhakikisha inapambana na matumizi mabaya ya fedha katika uchaguzi na nafasi tulizo nazo kutozitumia kutafuta madaraka.”

Alisema watu wanaokamatwa wakitumia fedha kupata madaraka wanatakiwa kukatwa kabisa na chama hicho kuwania nafasi hiyo.

“Kiongozi anayetumia fedha kununua uongozi hawezi kupambana na rushwa hawezi kuleta mabadiliko ya aina yoyote katika nchi hii,” alisema.

Alisema chama hicho kinatakiwa kujihadhari na watu wa aina hiyo kwa sababu Uchaguzi Mkuu ujao ni muhimu kuliko chaguzi zote za miaka ya nyuma kwa sababu ni uchaguzi ambao utaamua mwelekeo wa Tanzania.

“Tanzania ipo njiapanda. Nasema hivi kwa sababu mambo yote ya kuiwezesha nchi kufanya vizuri yapo, uchumi unakua vizuri, gesi inakuja, amani kidogo na utulivu upo, ina vijana wengi wenye hamasa, kilimo tunaweza kukipanua, ufugaji kuuboresha,” alisema.

Aliongeza, “Kuna njia nyingine ya kuchukua baada ya kuwapo kwa nyufa nyingi. Kuna tatizo la ajira, lipo suala la Muungano pamoja na rushwa ndiyo maana nasema uchaguzi ujao ni muhimu. Uchaguzi huo ndiyo hatima ya Tanzania tuipendayo.”

Akizungumzia sifa za rais ajaye Makamba alianza kwa kueleza nia yake ya kutaka nafasi hiyo na kusisitiza kuwa sifa anazo na hatanii katika hilo kama ambavyo watu wengi wanavyodhani kuwa ana malengo ya baadaye na si sasa.

Alisema kila kizazi cha uongozi wa Tanzania kina changamoto zake na kusisitiza kuwa hivi sasa Tanzania inatakiwa kuwa na kiongozi anayetoka katika kizazi kinachotizama mambo ya mbele, si yaliyopita.

“Kama watu wamefarakana na kugombea uongozi huko nyuma siyo sababu ya kutafuta uongozi ili kulipiza kisasi na kuendeleza mafarakano yao.

Kuna dhana kwamba uongozi ni kupokezana kijiti kutoka kizazi kimoja kwenda kizazi kingine, sasa ni wakati wa kupokezana kijiti kutoka kwao kuja kwetu,” alisema.

Alisema rais anatakiwa kuwa mtu asiye na doa la rushwa, awe na uelewa mpana kuhusu mazingira ya nchi yetu yaliyopo sasa, changamoto za watu kwa kawaida na uelewa mpana kuhusu dunia ilivyo, kwani Rais ajaye atajihusisha na ulimwengu, huku akimtolea mfano Rais Jakaya Kikwete.

“Awe na uwezo wa kuwaunganisha Watanzania kwa sababu kama mnavyoona chembechembe za mgawanyiko zimeanza, mgawanyiko kati ya Tanzania bara na Tanzania Visiwani, mgawanyiko wa kidini na kikanda,” alisema na kuongeza;

“Awe kiongozi mtendaji, kwa sababu sisi tunazo sheria, mifumo na mipango, lakini shida ni utekelezaji na kwa kiongozi tunayemtaka ni yule ambaye hatakuwa mbali na mifumo ya utekelezaji. Si kiongozi anayetoa hotuba na maelezo mazuri tu, bali kuhakikisha kiongozi ambaye atatoa adhabu kwa wale ambao watashindwa kutekeleza yale ambayo tumekubaliana,” alisema.

Alisema taifa halihitaji kiongozi ambaye amewahi kukaa Serikali kwa miaka 30 hadi 45, kusisitiza kuwa zama hizi zinahitaji rais mwenye sifa nyingine za ziada.

Alisema kwa hali ilivyo sasa, bado CCM ni chama sahihi kinachotakiwa kutoa rais katika uchaguzi ujao kutokana na historia ya chama hicho pamoja na viongozi na makada wake.

“Nchi ina changamoto nyingi lakini mambo yaliyofanywa na CCM yanaonekana. Chama kina historia ya uongozi barani Afrika na misimamo ambayo chama kimeuchukua katika ukombozi wa mtu mweusi ni historia ya kujivunia sana,” alisema.

Alisema chama hicho kina watu wa aina mbalimbali na kina uwezo wa kutoa viongozi wazuri, “CCM kinasimamia sera sahihi, nzuri na bora kwa maendeleo ya mtu. Ukitaja kila kitu, mfano katika kilimo tuna msimamo na sera na mipango kwenye afya. Hivyo hivyo katika kilimo, afya, elimu na maji.”

Akizungumzia elimu alisema, “Mfumo wetu wa elimu lazima tuufumue upya ili tumweke mwalimu na mwanafunzi katikati ya mazingira mazuri ya mipango yetu ya elimu.”

Alisema bila ya mwalimu aliyeridhika nchi haiwezi kupiga hatua, kusisitiza kuwa walimu waliopo lazima walipwe vizuri, kuondoa dhana kwamba ualimu ndiyo fani ya kukimbilia watu wanapokosa pahara pa kwenda.

“Kuanzisha ukaguzi, malipo, mitalaa, katika mambo ya kuongoza taifa hili hakuna ambacho sijafikiria katika kulifanya. Lazima tuamue lugha yetu ya kufundishia iwe ipi kwani mwaka 2007 ulifanyika utafiti na kubaini mwanafunzi wa sekondari walishindwa kusoma na kutafsri aya ndogo tu ya Kiingereza ya shule ya msingi na mimi naamini kwamba tunaweza kuziweka lugha zote zikatumika,” alisema.

Alisema mwalimu mwenye motisha anaweza kusaidia kuboresha elimu na mabadiliko ya mitalaa kutokana na uongozi.

Ajira

Akizungumzia tatizo la ajira nchini, Makamba alitaja mipango madhubuti ambayo kama ikifanyika itamaliza kabisa tatizo la ajira nchini.

“Hivi sasa kuna vijana 900,000 wa kati ya miaka 15 na 24 wanaingia katika soko la ajira kila mwaka. Watu waliopo katika soko la ajira ni karibia milioni 22 na idadi hiyo itaongezeka mara mbili katika miaka 15 ijayo. Mwaka 2030 tutakuwa na watu milioni 45 katika soko la ajira na hao ni watu wengi mno,” alisema.

Alisema jambo la kwanza ni kurekebisha mfumo wa elimu ambao utawawezesha vijana kuwa na uwezo na maarifa ya kupata ajira zinazoendana na uchumi wa kisasa, kutokana na sasa nchi kuwa na vijana wengi wasiokuwa na maarifa ambao wameishia darasa la saba au kidato cha nne.

“Tunaweza tukatenga Sh3 trilioni au Sh4 trilioni kwa ajili ya uwekezaji. Hizi fedha tunaweza kuzipata. Tuanze kwa kufufua viwanda 11 vya nguo vilivyokufa. Tanzania tunalima sana pamba lakini pamba inayotumika katika viwanda vya Tanzania ni asilimia 30 tu, asilimia nyingine yote inauzwa nje,” alisema.

Alifafanua kuwa kama nchi ikiweza kutumia asilimia 70 ya pamba inayozalishwa katika viwanda vya ndani itakuwa imetoa ajira kubwa.

Alisema ajira pia inaweza kuongezwa katika sekta ya kilimo ambayo inaajiri watu wengi nchini kwa kuongeza thamani ya mazao.

“Kuongeza thamani siyo kitu kikubwa, mfano kukamua juisi ni kuongeza thamani, kutengeneza maboksi na kupaki vizuri matunda ni kuongeza thamani na kukoboa mahindi na kutengeneza unga wa sembe ni kuongeza thamani,” alisema.

Pia, alitolea mfano jambo jingine na kupunguza tatizo la ajira kuwa ni kuweka mikakati ili Mifuko ya Hifadhi za Jamii, kuanzisha mifuko mikubwa ya kutoa mikopo na dhamana kwa wajasiriamali.

“Jambo jingine, ununuzi unaofanywa na Serikali. Kila siku serikali inanunua karatasi, vipuri, mafuta, tiketi za ndege, chakula, maji ya kunywa na mengine mengi. Unaweza kuweka utaratibu kwamba asilimia 30 ya ununuzi wa serikali uende kwenye kampuni ndogondogo za vijana na akina mama ili kuwajengea uwezo,” alisema.

Alisema katika miji yote na vijijini, chimbuko lake la uchumi ni biashara ndogondogo, lakini hakuna taasisi au mamlaka mahsusi inayojihusisha na kusaidia biashara ndogondogo.

Alisema, “Jambo jingine ni vyuo vya ufundi. Huko nyuma tuliahidi kwamba kila wilaya itakuwa na chuo cha ufundi na tunafahamu kuwa mfumo wetu wa elimu vijana wengi wanamaliza darasa la saba na kidato cha nne, hawaendelei na elimu ya juu. Elimu wanayoipata haiwasaidii kufanya shughuli yoyote au kupata kazi.”

Aliongeza, “Watu hawa wote wanatakiwa kuchukuliwa na vyuo vya ufundi ili kujifunza stadi za maisha kama ufundi selemala au ufundi ujenzi. Utaratibu ni kwamba utakapomaliza chuo katika wilaya zetu, kama wewe ni fundi selemala unaondoka na vocha ya kukuwezesha kupata vifaa ili kuanza biashara ya ufundi uliousomea.”

Alitolea mfano nchi Ujerumani kuwa wana mfumo mzuri wa elimu, kufafanua kuwa magari wanayotengeneza ya nchini humo aina ya Mercedes Benz, asilimia 70 ya vifaa vinavyotengeneza magari hayo, vimetengenezwa na kampuni ndogo za watu ambao hawakufika vyuo vikuu.

“Hata kwetu tuna vyuo vya ufundi 150, sasa kama vikiwa vinatoa watu wenye ujuzi na uwezo wa kufanya kazi za mikono na kuzalisha mali faida yake kwa soko la ajira na uchumi itakuwa kubwa sana,” alisema.

Alisema, “Siku hizi kuna misamaha ya kodi ambayo mtu hupewa kwa kuja tu nchini. Misamaha ya kodi inatakiwa kubadilishwa na kuwekewa kigezo kingine. Kama wewe ukiweza kuajiri watu 1,000 kwa kadri utakavyoongeza watu 1,000 katika biashara yako unapata mwaka mmoja wa msamaha wa kodi, ukiongeza 2,000 utapata msamaha kwa miaka miwili.”

Ataja mali zake

Akitaja mali zake Makamba alisema, “Katika vitu ambavyo havinisumbui kabisa ni suala la kumiliki mali, huwa ninapata lawama kubwa kwa ndugu na jamaa kwamba nina nafasi, lakini sina miradi mikubwa wala biashara. Mimi sivyo nilivyo, mimi maisha ya kuishi kwa mshahara na posho.”

Alisisitiza, “Kijijini nina kashamba kadogo, nina gari ambalo anatumia mke wangu na tuna nyumba ambayo tulipewa zawadi wakati wa harusi yetu. Sina biashara yoyote ambayo ninaendesha na sijawahi kufikiria kujilimbikizia mali na hii haijalishi kama nipo au sipo katika uongozi.”

Advertisement