Makamba azindua kampeni ya upandaji miti Mlima Kilimanjaro

Muktasari:

Kampeni ya kuchangia upandaji miti imezinduliwa leo Jumatatu jijini Dar es Salaam, ikiwa na lengo la kuhamasisha kila Mtanzania kupanda mti mmoja kwa mwaka.

Dar es Salaam. Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, January Makamba amezindua kampeni ya kuchangia upandaji miti kuzunguka Mlima Kilimanjaro na maeneo mengine ya mkoa huo.

Kampeni hiyo iliyozinduliwa leo Jumatatu Novemba 19, 2018 inayofahamika kama ‘Tuje Pamoja Challenge’ inalenga kuwahamasisha Watanzania kupanda angalau mti mmoja au kuchangia kuwezesha mti kupandwa.

Kiongozi wa mradi huo wa Kilimanjaro, Sarah Scott amesema endapo kila Mtanzania atapanda mti mmoja nchi itapiga hatua kwenye suala la mazingira.

Amesema pamoja na mambo mengine kampeni hiyo inalenga kuwajengea Watanzania utamaduni wa kupanda miti na kurejesha misitu iliyopotea.

“Lengo letu ni kuwafanya wananchi waone faida ya kutunza miti badala ya kuikata na tumeamua kuendesha kampeni kwa mtindo wa kuchangia mti mmoja Sh3,000 na miti miwili Sh10000. Fedha ambazo zinatumwa kwenye namba maalum,” amesema.

Kwa upande wake Waziri Makamba amesema suala la uharibifu wa misitu ni changamoto ambayo wamekuwa wakihangaika kuipatia ufumbuzi hivyo anafarijika kuona taasisi au watu binafsi wakiweka nguvu zao kwenye suala hilo.

“Ni faraja kwetu kuona watu au taasisi binafsi zinavalia njuga suala hili, Tanzania tumebarikiwa kuwa na eneo kubwa la Misitu Afrika Mashariki lakini tunaongoza katika kuiharibu hiyo misitu,” amesema Makamba.