Makamu wa Rais akemea upangaji safu za uongozi CCM

Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan akizungumza mjini Babati jana, kulia ni Waziri wa Tamisemi Selemani Jafo na kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Manyara Alexander Mnyeti. Picha na Joseph Lyimo

Muktasari:

Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan amewaonya wana CCM  wanaopanga safu za viongozi ndani ya chama hicho kwa ajili ya uchaguzi ujao kuwa watachukuliwa hatua kwa kukatwa majina yao wakibainika

Babati. Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan amekemea vikali baadhi ya viongozi nchini wanaopanga safu kwenye chaguzi za CCM ili waweze kuchaguliwa katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.

Suluhu ameyasema hayo jana jioni Ijumaa Novemba 16, 2018 kwenye uwanja wa Kwaraa mjini Babati mkoani Manyara akizungumza na wananchi wa eneo hilo.

Amesema viongozi wote wanaopanga safu yao ili waweze kuchaguliwa kwenye ngazi ya udiwani na ubunge watawachukulia hatua pindi ikigundulika wamefanya hivyo.

"CCM ni moja, hivyo hakuna haja ya kupanga safu kwenye ngazi za chini ili uweze kuchaguliwa katika udiwani au ubunge, tukigundua tu tunaondoa majina yao," amesema.

Amewataka wanachama wa chama hicho kujipanga ipasavyo kwa kujiandaa kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka 2019 ili waweze kushinda kwa kishindo.