Makanisa yagombea umiliki Chuo Kikuu cha Mount Meru

Mwenyekiti wa wachungaji wa makanisa wanachama wa Jumuiya kuu wa Wabaptist Arusha Fredrick Mahanyo akiwa na wachungaji wenzake wakizungumza na waandishi juu ya umiliki wa chuo kikuu cha Mount Meru na kudai kimetekwa na kanisa la Wabastisti Tanzania  kulia ni mchungaji Justine Mollel. Picha Mussa Juma

Muktasari:

Muungano wa makanisa wanachama wa jumuiya kuu ya Wabastisti Tanzania na Kanisa la Bastisti Tanzania umeingia katika mgogoro wa kugombea umiliki wa Chuo Kikuu cha Mount Meru Arusha ambacho sasa kimefungwa  kutokana kushindwa kukidhi matakwa ya Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU).

Arusha. Wachungaji  wa makanisa  wanachama wa Jumuiya Kuu ya Wabaptisti Tanzania wameomba Serikali kuwasaidia kuwarejeshea umiliki wa Chuo Kikuu cha Mount Meru kilichopo wilaya ya Arumeru mkoani Arusha.

Chuo hicho ambacho kimekumbwa na migogoro na kusababishwa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) kukisitisha kufanya usaili, kwa sasa kinaendeshwa na Askofu Mkuu wa Kanisa la Baptisti Tanzania, Anold Manase.

Wakizungumza na waandishi wa habari leo, wachungaji wa makanisa ya jumuiya kuu ya Wabaptist  Tanzania walisema chuo  kikuu hicho kilianzishwa mwaka 2012 na taasisi tano ambazo ni jumuiya kuu wa Wabaptisti ya Kenya na Muungano wa Baptisti Uganda.

Taasisi nyingine ni International Mission Board ya  jumuiya kuu ya Wabaptisti ya Marekani ambapo awali chuo hicho kilikuwa kikitumika kutoa mafunzo ya dini pekee.

Mwenyekiti wa umoja wa machungaji ya jumuiya kuu ya wabaptisti Arusha, Mchungaji Fredrick Mahanyo alisema kanisa la Baptisti Tanzania siyo wamiliki wa chuo hicho.

"Askofu Manase ameteka uongozi wa chuo na ameanzisha hilo kanisa lake ndani ya taasisi na hivyo kusababisha chuo kuzuiwa kufanya udahili kutokana na kushindwa kufikia vigezo wa TCU" alisema

Hata hivyo, Askofu Manase alikanusha kuteka chuo hicho na kueleza wanaomtuhumu wanapaswa kutoa vielelezo vya umiliki wa chuo hicho.

"Hao wachungaji ni kina nani, kuna baptisti nyingi, tuna Bible Baptisti na Baptist Convention, hao ni nani nani, kama wana ushahidi wakupe nyaraka sisi tuna taratibu zetu," alisema

Mchungaji mwingine wa jumuiya hiyo, Justine Mollel alidai tangu askofu huyo achukue uongozi katika chuo hicho mwaka juzi, kumekuwapo uzembe wa watendaji ofisi ya taaluma, wizi wa vyeti vya chuo na wanachuo kupewa matokeo ya uongo.

"Wafanyakazi wanapolalamika wengi wameachishwa kazi lakini pia uongozi wa chuo umekuwa ukiingilia uongozi wa kanisa  la Baptisti Tanzania ambalo halijasajiliwa nchini" alisema.

Mchungaji Alphayo Michael alisema wanaomba Serikali kuingilia kati kutatua mgogoro huo kwani wanafunzi waliokuwa wanasoma chuo hicho wanataabika na wafanyakazi.

"Jumuiya kuu ya Wabaptist hatuna cheo cha askofu lakini kuna mtu anajiita askofu na amekiteka chuo na kukifanya ni mali yake kupitia kanisa lake la Tanzania Baptisti ambalo halijasajiliwa nchini" alisema

TCU Septemba 20, 2018 ilikifungia chuo cha Mount Meru kutokana na kushindwa kutimiza masharti, ikiwamo kutakiwa kuongeza walimu, kurekebisha maabara na kuwalipa watumishi stahili zao.

Chuo cha Mount Meru hadi kinasitishiwa usaili kilikuwa na zaidi ya wanafunzi 200 ambao tayari wote wameondolewa na walimu 60 ambao hadi sasa wamesimamishwa kazi kutokana na chuo kufungwa.