Makonda awagusia waliotajwa na Magufuli

Muktasari:

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amesema kazi kubwa inafanyika kukabiliana na wafanyabiashara ambao juzi Desemba10, 2018 Rais John Magufuli alisema wanaingiza makontena kutoka nje kwa niaba ya wenzao lakini hawalipi kodi na kuikosesha Serikali mapato.

Dar es Salaam. Baada ya juzi Rais John Magufuli kusema kuna wafanyabiashara wanaoagiza mizigo kutoka nje kwa niaba ya wenzao kisha kukwepa kodi, mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amesema kazi kubwa inaendelea kufanyika ili kukabiliana nao.

Juzi, Rais alisema kuna wafanyabiashara wanaoingiza makontena kutoka nje kwa niaba ya wenzao, lakini hawalipi kodi hivyo kuikosesha Serikali mapato.

“Wapo wawili, mmoja jina lake linaishia na agency na mwingine lina o mwishoni. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam upo na TRA ipo, hamjui hili?” alihoji Rais Magufuli.

Juhudi za kuwapata wasemaji wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), mpaka tunakwenda mitamboni ili kupata ufafanuzi kuhusu taarifa alizonazo Rais hazikuzaa matunda.

Kuhusu wafanyabiashara wanaokwepa kodi kwa kuwatumia wamachinga, mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Kariakoo (JWK), Philimon Chonde alisema wameshalifikisha suala hilo TRA mara kadhaa hivyo linahitaji ufuatiliaji.