Mali za rushwa kutaifishwa

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  akizungumza na Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Paramagamba Kabudi (katikati ) na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapteni  (mstaafu), George Mkuchika baada ya kuhutubia katika Kilele cha Maadhimisho ya Maadili na Haki za Binadamu jijini Dodoma jana.Picha na Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu

Muktasari:

Tanzania iko nafasi ya 14 kati ya nchi 54 Afrika iki-panda nafasi tatu kutoka 17 ya 2017 katika utawala bora, kwa mujibu wa Waziri George Mkuchika .

Dodoma. Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Diwani Athuman amesema wanapambana na watu waliojitajirisha kupitia rushwa na kila mtumishi wa umma anachuguzwa kujua kiwango cha kipato chake na mali anazomiliki.

Athuman amesema uchunguzi huo unalenga kujua namna watumishi hao wanavyozingatia misingi ya utumishi na kwamba, ikibainika kuwa mtuhumishi amejipatia fedha kwa njia za rushwa mali yake itataifishwa.

Akizungumza katika kilele cha maadhimisho ya siku ya maadili na haki za binadamu yaliyofanyika jijini hapa jana, alisema, “Ukiwa na mali iliyotokana na rushwa usidhani uko salama, wakati wowote watoto wako watashangaa wakikosa mali.”

Awali, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliutaja mgongano wa masilahi katika ngazi ya halmashauri kuchangia hasara kubwa kwa Serikali tangu muda mrefu kutokana na uamuzi usiokuwa na maadili ambao mwingi huwa na viashiria vya rushwa.

Alisema mara kadhaa baadhi ya viongozi wamekuwa wakitoa uamuzi ambao unakuwa umebeba viashiria vya rushwa na ukiukwaji wa maadili, lakini bado wanafumbiwa macho na kuendelea kuiumiza Serikali.

Alisema pia wapo baadhi ya watumishi na madiwani wanaotoa uamuzi unaohitimishwa kwa kumpatia kazi mkandarasi au mzabuni wakati kampuni husika inamilikiwa na mwenza, rafiki, ndugu au mtoa rushwa.

“Mambo hayo yamechangia rasilimali za Taifa kuwanufaisha wachache wakati wengine wanaendelea kuwa mafukara,” alisema Majaliwa.

Pia alizinyooshea kidole idara za manunuzi kuwa kichaka cha kutafuna fedha na kwamba, Serikali inakusudia kufanya maboresho katika eneo hilo.

“Serikali haitamvumilia mtu yeyote mvunjaji wa sheria na mla rushwa tutashughulika naye bila huruma. Haya mambo yanatakiwa kuangaliwa kuanzia ngazi ya chini hadi nafasi za juu, nawakumbusha Watanzania kuwa jambo hili tupambane kwa pamoja katika kurejesha maadili.”

Katika hatua nyingine alisema Serikali inaendeleza mapambano makini dhidi ya rushwa ikiwemo kuanzishwa kwa mahakama ya makosa ya rushwa kunakokwenda sambamba na kuongeza adhabu za wanaotiwa hatiani.