Malkia Karen: Nilianza kuimba nikiwa na miaka 7

Muktasari:

Huyu si mwingine bali ni Karen Gardner, mtoto wa mtangazaji maarufu nchini Gardner G. Habash ambaye kwa sasa anafanya kazi katika kituo cha Clouds.

Miezi nane iliyopita aliachia kibao kinachokwenda kwa jina la Tunaendana, ikiwa ni mara yake ya kwanza kujitambulisha kwenye tasnia ya muziki.

Huyu si mwingine bali ni Karen Gardner, mtoto wa mtangazaji maarufu nchini Gardner G. Habash ambaye kwa sasa anafanya kazi katika kituo cha Clouds.

Kwani akiwa na nyimbo tatu tu mpaka sasa, achilia mbali Tunaendana ipo lawama na Washa aliyoiachia wiki moja iliyopita, baadhi ya watu wanahisi huenda jina lake limejulikana haraka kupitia umaarufu wa baba yake.

Katika mahojiano kati yake na gazeti la Mwananchi amefunguka mengi aliyoyapitia kabla hajaanza muziki.

Mwandishi: Lini hasa ulijitambua kuwa una kipaji cha kuimba

Karen: Nikiwa na miaka saba niligundulika kuwa na kipaji cha kuimba

Mwandishi: Nani ulikuwa ukimwangalia katika tasnia ya muziki

Karen: Niliyekuwa nikiwangalia zaidi wasanii wa Marekani akiwemo Brandy, na kundi la TLC, vipindi vya muziki vya ITV jioni nikawa naigiza nyimbo na kucheza.

Mwandishi: Baba yako ni mtangazaji wa siku nyingi na anajua soko la muziki, je ana msaada gani kwako

Karen: Baba yangu nakiri ni nguli wa muziki, amekuwa akinisaidia wakati wa kwenda kwenye shoo au kwa ajili ya mahojiano kumwambia vipi vya kuongea na vipi sio vya kuongea.

Pia ananisaidia kifedha katika kufanya kazi zangu mbali na menejimenti yangu kusimamia mambo mbalimbali.

Mwandishi: Ulishawahi kukuweka chini na kufundwa kuhusu yaliyomo kwenye muziki

Karen: Kuhusu kufundwa sio tu wazazi wangu wanaonifanyia hivyo kwani kazi hiyo hufanywa na ndugu jamaa na marafiki pamoja na wasanii walionitangulia kwenye kazi hiyo ya muziki.

Mwandishi: Lady Jay Dee ni kati ya wasanii wakubwa wa kike, je, ulishawahi kuwaza kufanya naye kazi na je ana mchango wowote katika kazi yako

Karen: Lady Jay Dee ni kati ya watu waliogundua kipaji changu nikiwa mdogo, kuhusu kufanya naye kazi kila kitu ni mipango kwani hata hilo linawezekana halina shida.

Mwandishi: THT imepika vipaji vingi je ulishawahi kwenda kupata maujuzi ?

Karen: THT ni kweli nipo huko kwani wasimamiaji wa kazi zake Epic Records ndipo walipo hivyo wana mchango mkubwa katika kipaji chake

Mwandishi: Awali kulitokea tetesi kuwa una uhusiano na Petit Man, hili limekaajae na je lina ukweli wowote?

Karen:Suala la Petit halina ukweli wowote, kwani tulikuwa tunafanya tu video na hakuna chochote kinachoendelea kati yetu kwa sasa kama watu wanavyosema.

Mwandishi: Kwa mara ya kwanza ulijuana na Petit wapi na mahusiano yenu kwa sasa yakoje?

Karen: Petit nilianza kumjua kupitia mitandao, na mara ya kwanza nilionana naye uso kwa uso mwaka huu uwanja wa ndege wa Mwalimu Julius Nyerere akiwa ameenda kumpokea msanii wake Country Boy.

Nilipokwenda kumsalimia msanii mwenzangu huyo ndio hapo tukazungumza mengi ikiwemo kuanzisha wazo la kufanya naye kazi.

Mwandishi: Baada ya taarifa hizo kuzagaa wazazi wako walilichukuliaje

Karen: Haikuniletea matatizo kwa wazazi kwa kuwa watu wangu wengi wa karibu walikuwa wakijua kuwa ni mtu ninayefanya naye kazi.

Mwandishi: Video zako ni za kiwango, hivi zote umezifanyia hapa Bongo au kuna nyingine umezifanyia nje ya nchi?

Karen: Pamoja na ubora wa video zangu kama mnavyoziona, hakuna niliyoifanya nje ya nchi zote nimezifanyia hapa nchini tena Dar es Salaam.

Mwandishi: Kutokana na kuwa msanii ambaye una baba anajulikana, vipi ushapata usumbufu kutoka kwa wasanii wengine wanaotaka kutoka au waliopo kwenye tasnia kuomba uwasaidie

Karen:Ni kweli nimekuwa nikipata usumbufu wa watu kutaka niwasaidie kumtoa kimuziki.

Japokuwa wanapaswa kujua kwamba hata mimi nimetoka sio kwa jina la baba yangu bali kwa juhudi zangu na nimepitia ambayo wanapitia wengine ili kuthibitisha kwa jamii kwamba una kipaji.

Mwandishi: Je una mpango wowote wa kuachia albamu siku za usoni na kwa lini.

Karen: Suala la kutoa albamu bado, kwani bado watu hawajanijua kihivyo,

kwa hiyo kazi niliyonayo kwa sasa ni kutengeneza kwanza jina langu hivyo ataendelea kutoa nyimbo moja moja.