Mama Ardhi Alliance yazinduliwa Dar

Kaimu Mkurugenzi wa Kituo Cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Imelda Urio

Muktasari:

Mashirika hayo ni Chama Cha Wanasheria Wanawake (TAWLA), Chama cha Wanahabari Wanawake (TAMWA), Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) na Kituo cha Msaada wa Kisheria kwa Wanawake (WLAC).

Dar es Salaam.  Mashirika 10 ya kutetea haki za binadamu yamezindua mtandao wa haki kwa mwanamke katika kumiliki ardhi unaojulikana ‘Mama Ardhi Alliance’.

Mashirika hayo ni Chama Cha Wanasheria Wanawake (TAWLA), Chama cha Wanahabari Wanawake (TAMWA), Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) na Kituo cha Msaada wa Kisheria kwa Wanawake (WLAC).

Mengine ni Shirika la Wanawake Katika Sheria na Maendeleo ya Afrika (WILDAF), TAHEA, WAT, IDS na NOCHU.

Akizungumza baada ya kuzindua mtandao huo, Mkurugenzi wa Shirika la Woman Fund Tanzania, Mary Lusindi aamesema lengo la mtandao huo ni kutoa fursa kwa wanawake kumiliki ardhi.

“Kwa sasa serikali inakabiliwa na changamoto katika suala la umiliki wa ardhi kwa wananchi kutokana na jamii kutokuwa na uelewa wa sheria za kumiliki wa ardhi ususani wanawake,” amesema Lusindi.

Kaimu Mkurugenzi wa Kituo Cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Imelda Urio alisema lengo la mtandao huo ni kuhakikisha kuwa sheria za usimamizi wa ardhi zinatekelezwa ipasavyo ili ziweze kutoa nafasi kwa mwanamke kumiliki ardhi.

“Sheria zipo lakini tunaona hazitekelezwi, likija suala la usimamizi kunakuwa hakuna utekelezaji hivyo kupitia mtandao huu tutahakikisha kuwa mwanamke anapata haki ya kumiliki ardhi,” amesema Urio na kuongeza:

“Sheria za ardhi za kimila zinatambua mwenye haki ya kumili ardhi ni mwanaume pekee wakati sheria ya ndoa na sheria ya  mirathi zinatambua  mwanamke ana haki ya kumiliki ardhi,” mwanaharakati huyo ameongeza.

Urio ambaye ameteuliwa kuwa mwenyekiti wa wa mtandao huo (Mama Ardhi Alliance), amesema kutokana na changamoto mbalimbali walizoziona katika umiliki wa ardhi kwa wanawake ndio sababu ya wao kuanzisha mtandao huo ambao utawaokoa wanawake hususani wa vijijini.

Mkurugenzi mtendaji wa Tawla, Tike Mwambipile amesema lengo la kuanzisha mtandao huo unaohusisha mashirika 10 ni  kuangalia haki za wanawake katika kumiliki mali  na ardhi.