Mama Mobetto amzungumzia mchumba mpya wa mwanae

Muktasari:

Mama wa mwanamitindo Hamisa Mobetto, amesema hamtambui mchumba mpya wa mwanaye kwani naye anamuona mitandaoni

Dar es Salaam. Wakati moja ya habari ambayo imekuwa gumzo hivi karibuni katika mtandao wa kijamii wa ‘Instagram’ ni ile inayomhusu mchumba mpya wa mwanamitindo Hamisa Mobetto lakini mama wa mwanamitindo huyo amesema hamtambui.

Mchumba huyo anayejulikana kwa jina la Josh Adeyeye , alianikwa hadharani kwa mara ya kwanza na Hamisa Novemba 9, 2018 wakiwa wameshikana kimahaba na kuandika ‘Roho Mkalia Moyo’ ambapo watu takribani 154,000 waliyoiona picha hiyo wengi walimsifia mwanaume huyo na kudai wameendana.

Mwananchi limemtafuta mama wa mwanamitindo huyo, Shufaa Rutiginga, kujua ukweli kuhusu Josh na kama kuna hatua zozote zimeshaanza za kutambuliwa kwenye familia kama mkwe.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumatatu Novemba 20, mama huyo amesema hata yeye mchumba huyo anamuona kwenye mitandao kama watu wengine.

Shufaa amesema hamtambui kwa kuwa kiutaratibu katika mila za Kiafrika kuna kwenda kumtambulisha mchumba nyumbani, lakini hilo kwa Hamisa hajalifanya hadi sasa.

“Hapa naona kama unanikosea sana mwanangu kuniambia namtambua hawara wa mtoto wakati sijatambulishwa kama tamaduni zetu zinavyotaka, hebu nitake radhi.”

“Siku akija kutambulishwa rasmi na mhusika nitakuwa na nafasi nzuri ya kulizungumza hilo ila kwa sasa sina cha kusema,” amesema mama huyo.

Akizungumzia kuhusu nyimbo mpya ya mtoto wake aliyoiachia jana iitwayo ‘Tunaendana’  amesema ni nyimbo walikuwa wakiijua siku nyingi kama familia na wameiimba na kushika mashairi yake muda mrefu.

Isipokuwa kilichokuwa kinasubiriwa ni kutoka na video yake na kuongeza kuwa anashukuru hilo limefanikiwa tena kwa kupigwa picha zake nchini Marekani wakati awali mpango ilikuwa itengenezewe hapa nchini.

Amebainisha gharama za video hiyo zimewezeshwa kwa kiasi kikubwa na mashabiki wa Hamisa wanaoishi nchini Marekani huku akiwaomba watu kumpa sapoti mtoto wake ili aweze kufika mbali katika ndoto zake za kuwa msanii wa muziki.

Mbali na wimbo wa Madam Hero na huu mpya wa ‘Tunaendana’, mama Hamisa amesema tayari kuna nyimbo nyingine mbili zilizo tayari na kutarajiwa kuachiwa muda wowote.