Mambo 9 yatikisa Bunge

Muktasari:

  • Hoja ya kwamba Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Isack Kamwelwe ana dharau ni kati ya mambo tisa yaliyolitika Bunge katika mjadala wa Mpango wa Maendeleo mwaka 2019/20.

 

Dodoma. Mtindo wa wabunge kujivua uanachama na nyadhifa zote ndani ya chama chake na kuhamia kingine ulishazoeleka, lakini si kwa staili iliyotumiwa na Abdallah Mtolea; alitumia kikao cha Bunge la Jamhuri ya Muungano kutangaza uamuzi wake wa kujiondoa CUF.

Na tena alitumia mjadala wa Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2019/20 uliokuwa umepamba moto katika Mkutano wa 13 wa Bunge uliomalizika Ijumaa iliyopita mjini hapa.

Ilikuwa ni siku ya mwisho iliyotolewa na Kamati Kuu ya CCM kwa wabunge kutoka upinzani kutangaza kuhamia CCM, la sivyo watakaotangaza baadaye hawatapewa nafasi ya kugombea nafasi walizojivua, mtego ambao umenasa takriban wabunge kumi.

Kitendo hicho cha Mtolea aliyekuwa mbunge wa Temeke na ambayo hakuna shaka atapewa fursa ya kurudia kiti chake, ni moja ya mambo tisa yaliyogusa wengi katika mkutano huo wa Bunge ulioanza Novemba 6.

Wakati akichangia Mpango wa Maendeleo wa Taifa, ghafla Mtolea alihama kutoka hoja hiyo ya kitaifa na kuanza kuzungumzia uamuzi wake binafsi akisema umetokana na pande zinazosigana CUF.

“Tumekuwa tukisigana kiasi ambacho tumekuwa tukihatarisha maisha yetu mpaka mitaani. Muda wote mnakuwa katika hofu ya kufukuzwa. Hata mimi hapa, kwa taarifa ambazo zimeletewa, wakati wowote wiki ijayo ningefukuzwa,” alisema Mtolea aliyekuwa amevalia kaunda suti ya rangi nyeusi huku akishangiliwa kwa makofi.

“Sijui mnaoshangilia mnashangilia nini, lakini tulio ndani ndiyo tunaujua huu mgogoro.

“Najiuzulu nikiwa bado natamani kuwahudumia wananchi wa Temeke. Kwa hiyo nakaribisha vyama vyote kuanzia Chadema, NCCR na CCM kujadiliana namna tutakavyoweza kushirikiana.”

Baada ya kusema hayo alianza kutembea kuelekea nje ya ukumbi. Baadaye jioni, aliomba kujiunga na CCM na kuibua mijadala nje na ndani ya chombo hicho cha kutunga sheria.

CUF imekuwa kwenye mgogoro tangu Profesa Ibrahim Lipumba, aliyekuwa amejivua uongozi, arejee madarakani kwa madai kuwa barua yake ya kujiuzulu haikujadiliwa wala kupitishwa na Mkutano Mkuu.

CUF sasa ina kundi linaloongozwa na Profesa Lipumba na jingine linalomuamini katibu mkuu wake, Maalim Seif Sharif Hamad.

Baada ya kutoa kauli hiyo, Spika alimtaka kutoka nje ya ukumbi wa Bunge ambapo Mtolea alitii amri hiyo na kumpa mkono Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Ajira Kazi na Vijana, Jenister Mhagama, Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini huku Mbunge wa Tunduma (Chadema), Pascal Haonga akikataa kupewa mkono.

Wakati hayo yakiendelea, ilizuka taarifa nyingine kuwa mbunge wa Tandahimba (CUF), Katani Katani pia amejivua ubunge, hali iliyozua taharuki ndani ya Bunge hasa kwa wabunge wa Kambi ya Upinzani. Hata hivyo, mbunge huyo alikanusha baadaye kuwa hajahama chama chake na wala hatarajii.

Katani pia alitumia kikao hicho kutangaza msimamo wake wakati akichangia Mpango wa Maendeleo wa Taifa.

Mambo mengine yaliyotikisa ni pamoja na utekaji na mauaji, tuhuma dhidi ya Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Isack Kamwelwe kuwa ana dharau na orodha ya mawaziri na wabunge ambao wamekuwa hawahudhurii vikao vya Bunge.

Nyingine ni Sheria ya Takwimu, panguapangua ya wajumbe ilivyoathiri Kamati ya Viwanda, Biashara na Mazingira, wabunge wawili kutolewa nje ya ukumbi, upinzani kutoneshwa vidonda na Azimio la Mkataba wa Takwimu wa Afrika, mazingira mabaya ya biashara na mdahalo wa uchumi na siasa ulioandaliwa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Kuhusu Sheria ya Takwimu ya Mwaka 2015 na marekebisho yake ya mwaka 2018, Naibu Waziri Kivuli wa Fedha na Mipango aliitaka Serikali kufuta sheria hizo na kuwasilisha sheria mpya bungeni.

Silinde, ambaye pia ni mbunge wa Momba (Chadema), alisema kufutwa kwa sheria hizo kutaufanya Mkataba wa Takwimu wa Afrika kuwa na manufaa kwa Taifa.

Suala la ununuzi wa korosho lililotokana na wakulima kugomea bei iliyotakiwa na wafanyabiashara na kusababisha Serikali kuingilia kati, pia liliibua mjadala bungeni wakati wa kujadili Mpango wa Maendeleo wa Taifa.

Waliochangia hoja hiyo ni pamoja na Hussein Bashe, mbunge wa Nzega Mjini (CCM), Hamidu Bobali (Mchinga-CUF) na Tulia Malapo (Viti Maalum, Chadema).

Wengine waliozungumzia ni Katani Katani (Tandahimba-CUF), Abdalah Chikota (Nanyamba-CCM), Ahmed Shabiy (Gairo-CCM), Nape Nnauye (Mtama-CCM) na Peter Serukamba (Kigoma Mjini- CCM) ambaye alishauri nguvu ya soko kuachwa itawale badala ya Serikali kuingilia kati.

Mbunge wa Ilala (CCM), Mussa Zungu aliishauri Serikali kuangalia mazingira ya biashara nchini ambayo yamekuwa yakisababisha wafanyabiashara kukimbia nchini.

Peter Msigwa alihoji ni kwanini Serikali haitaki kumwambia mfanyabiashara Mohammed Dewji ‘Mo’ aliyetekwa na watu wasiojulikana na kisha kurejeshwa na kutelekezwa auambie umma alifichwa wapi.

Lakini Josephine Gezabuke (Viti Maalum-CCM) na Mbunge wa Kigoma Kusini (CCM)

Husna Mwilima aliibuka na hoja ya kupinga kuvuliwa vyeo maofisa wa polisi na wengine kuhamishwa, ni kuwaonea.

Hoja hiyo ilitokana na amri iliyotolewa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola kutokana na mapigano yaliyotokea wilayani Uvinza baina ya wananchi na polisi.

Gezabuke alisema askari hao hawana nguvu ya kufanya jambo lolote, bali hupokea amri kutoka kwa wakubwa zao.

Hivyo aliitaka Serikali kuchukua hatua kwa watu wote waliohusika na vifo vilivyotokea. Katika mapigano hayo, wananchi wawili na polisi waliuawa.

Mohamed Mchengerwa (Rufiji-CCM), Ramadhan Dau (Mafia-CCM) na Seleman

Bungara ‘Bwege’ (Kilwa Kusini-CUF) walilamikia majibu yanayotolewa na

Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Mhandisi Isack Kamwelwe kuwa wakati mwingine yanaonyesha dharau.

Bungara alisema majibu hayo yanaonyesha dharau hata kwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ambaye yeye ameteuliwa na Rais John Magufuli na kisha kuthibitishwa na Bunge, tuhuma ambazo Kamwelwe alisema hazina ukweli.

Sakata hili lilitokana na wabunge hao kutoridhishwa na majibu aliyoyatoa bungeni kuhusiana na kero zilizoko katika majimbo yao zilizoshindwa kutatuliwa, licha ya kutolewa maagizo mara kadhaa na Waziri Mkuu.

Hoja ya kuwakosoa maprofesa walioshiriki katika mdahalo wa uchumi na siasa uliondaliwa na UDSM, nayo ilizua mjadala mzito bungeni.

Mbunge wa kwanza kukosoa alikuwa Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ (Mbeya Mjini - Chadema) akifuatiwa na Joseph Kasheku ‘Msukuma’ (Geita Vijijini-CCM).

Wabunge hao walisema maprofesa hao hawakulitendea haki Taifa na kwamba,

mada zao zilikuwa zikirudia hotuba za Rais John Magufuli.

Hoja iliyofunga kazi ilikuwa ni ile iliyotolewa na Spika Job Ndugai pale alipoamua kutoa taarifa ya mahudhurio ya wabunge katika vikao vya kamati na Bunge kwa mikutano ya Machi, Agosti

na Oktoba mwaka huu.

Aliwataja mawaziri watano kuwa ni miongoni mwa wabunge watoro na mahudhurio yao ni chini ya asilimia 50 ya vikao 33 vya kamati na 70 vya mikutano hiyo miwili.

Mawaziri hao na asilimia za vikao walivyohudhuria kuwa ni Waziri wa

Katiba na Sheria Profesa Palamagamba Kabudi (38), Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, January Makamba (37) na Waziri wa Mambo ya nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Augustine Mahiga.

Ndugai pia aliwataja wabunge aliodai kuwa ni watoro walio na mahudhurio ya chini kabisa ni pamoja na Salum Khamis Salum (Meatu-CCM), Mansoor Hiran (Kwimba-CCM), Abdulazizi Abood (Morogoro-CCM) Hussein Amar (Nyang’hwale-CCM), Mbaraka Bawazir (Kilosa-CCM) na Dk Mathayo David (Same Magharibi-CCM).

Wengine ni John Mnyika (Kibamba-Chadema), Salim Hassan Turky

(Mpendae-CCM), Suleiman Nchambi (Kishapu-CCM) na Mbunge wa Arusha

Mjini (Chadema), Godbless Lema ambaye alisema ndiye mbunge mtoro kuliko wote.

Pia katika mkutano huu, Spika Ndugai alipangua wajumbe wa kamati na wajumbe saba wa kamati ya Viwanda, Biashara na Mazingira, walipangiwa kamati nyingine.