Mambo mawili askari aliyejiua

Muktasari:

Askari huyo anadaiwa kujiua kwa kile alichodai tumbo linamsumbua kwa miaka mingi, RPC asema pia walimfungulia jalada la kumtia mimba mwanafunzi

Serengeti. Yohana Tangawizi, askari wa Gereza Mradi Tabora B wilayani Serengeti, aliyejiua kwa kujipiga risasi ameacha maswali mawili ya nini hasa sababu za kuamua kujitoa uhai.

Tangawizi aliyekuwa na cheo cha sajenti katika ujumbe aliouacha juzi, alidai anafanya hivyo kwa sababu ameugua kwa muda mrefu ugonjwa wa tumbo.

Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Juma Ndaki akizungumza na Mwananchi kwa simu jana, alisema pamoja na ujumbe wa maandishi alioua pia alikuwa amefunguliwa jalada la kumpa mimba mwanafunzi wa sekondari.

Jalada hilo linamhusisha Tangawizi na tuhuma za kumpa mimba mwanafunzi wa kidato cha pili katika Sekondari ya Kisangura.

Askari huyo alijiua kwa kujipiga risasi mbili mdomoni na kutokea kisogoni kwa kutumia bunduki aina ya SMG nyumbani kwake Novemba 8, saa tisa alasiri baada ya kutoka lindoni.

Kamanda Ndaki alisema, “Kabla ya kujiua alikuwa lindo la wafungwa, baada ya kufika nyumbani kwake aliwakuta watoto wake, mke hakuwepo, akawatuma kwenda kununua soda huku nyuma akajiua na kuacha ujumbe wa maandishi.”

Alisema kwenye ujumbe aliouandika, Tangawizi alisema amejiua kwa sababu afya yake ilikuwa inazorota kutokana na kuugua tumbo kwa muda mrefu licha ya kwenda kwa waganga wa kienyeji na hospitali.

Katika ujumbe huo, alisema ameamua kujiua na kutaka akazikwe ukweni Nyamuswa badala ya Kahama alikozaliwa. “Siku ambayo amefunguliwa jalada la kumpa mimba ndiyo aliyojiua, inawezekana kukawa na uhusiano wa hili pia maana inawezekana alijua atakamatwa.”