Mangula: Tafiti zisaidie jamii

Makamu Mwenyekiti wa CCM, Philip Mangula

Muktasari:

  • Mangula amewataka wasomi kufanya tafiti zinazojibu changamoto zilizopo kwenye jamii

Morogoro. Makamu Mwenyekiti wa CCM, Philip Mangula amesema tafiti nyingi zinazofanywa na wasomi zimekuwa kama rejea za wataalamu hao na si kujibu changamoto na matatizo ya jamii.

Mangula ameyasema hayo leo wakati akifungua kongamano la kumkumbuka Mwalimu Julius Nyerere ikiwa ni miaka 19 tangu afariki duniani lililoandaliwa na Chuo Kikuu Mzumbe kilichopo mkoani Morogoro.

Amesema kuwa wakati nchi ikikumbuka mchango wa Mwalimu Nyerere ni vyema taarifa za elimu ya juu zikawaandaa wahitimu wa elimu ya juu kuwa waadilifu ili waweze kulitumikia taifa katika nyanja mbalimbali.

Akieleza mitazamo ya Mwalimu Nyerere, Mangula amesema aliweza kutumia taaluma yake ya ualimu kulifundisha taifa mambo mbalimbali ukiwemo usawa, haki na wajibu huku akiamini elimu kuwa ni nyenzo muhimu katika kuielimisha jamii.

Mmoja wa watoa mada katika kongamano hilo ambaye pia ni makamu mkuu wa Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (Sua) Profesa Raphael Chibunda amesema kuwa mchango wa Mwalimu Nyerere kwenye sekta ya kilimo umeleta maendeleo makubwa kwa chuo hicho kwa kutoa wataalamu na watafiti wa kilimo.

Profesa Chibunda amesema Mwalimu Nyerere aliamini kukuza sekta ya kilimo kutawezesha mahitaji ya viwanda ambavyo alivianzisha katika mikoa mbalimbali ukiwemo mkoa wa Morogoro.

Ameshauri ili kumuenzi Mwalimu Nyerere lazima elimu ya juu ijikite katika kuwaandaa vijana ambao ni wahitimu wa vyuo vikuu kutumia taaluma zao katika kuipatia maendeleo nchi.

Naye Mkurugenzi wa TBC ambaye ni miongoni mwa watoa mada, Dk Ayoub Rioba amesema Mwalimu Nyerere alitumia vyombo vya habari kupinga ukandamizaji na kuibua mijadala.

Amewataka waandishi wa habari kujisomea machapisho mbalimbali yakiwemo ya Mwalimu Nyerere na kudumisha mila na desturi za Watanzania.