Marais waitwa kusaidia sakata la mafao

Katibu wa Chakamwata, Meshack Kapange

Dar es Salaam. Kama Serikali inadhani sakata la kanuni mpya za malipo ya pensheni limeanza kutulia, hali bado tete; marais wa zamani wanaombwa kushiriki kutafuta ufumbuzi.

Ombi la jana lilitolewa na Chama cha Kutetea Haki na Maslahi ya Walimu (Chakamwata), kikitaka Serikali iwakutanishe na watumishi wa umma, wakiwemo marais wastaafu ili kujadili sheria na kanuni mpya ya kikokotoo cha mafao hayo kwa wastaafu.

Katibu wa Chakamwata, Meshack Kapange aliwaambia waandishi wa habari jijini Mbeya kuwa sheria hiyo imepitishwa bila kushirikisha watumishi wa umma.

Alisema Serikali ilitumia vyama vya wafanyakazi ambavyo havina nia njema na watumishi.

Kapange alisema wamekuwa wakipinga kikokotoo hicho mara kwa mara wanapokutana na viongozi wa Tamisemi, wakiwaeleza ni kwa namna gani kanuni hiyo inawakandamiza walimu na watumishi wa umma.

“Tunaomba mjadala wa kikokotoo kipya kutokana na kwamba kinamfanya mtumishi wa Serikali ngazi ya kawaida kuwa maskini zaidi,” alisema Kapange.

Makamu mwenyekiti wa Chakumwata, Juma Issa alipendekeza Serikali kusitisha matumizi ya kikokotoo hicho kwa masilahi mapana ya nchi.