Mbowe, Matiko kuendelea kusota mahabusu

Muktasari:

Usikilizwaji wa rufaa ya kina Mbowe ulikwama baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), kukata rufaa Mahakama ya Rufani, akipinga uamuzi wa Mahakama Kuu kukubali kuisikiliza rufaa hiyo licha ya kuiwekea pingamizi la awali akitaka rufaa hiyo itupiliwe mbali.

Dar es Salaam. Wakati jana Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha) walisherehekea miaka 57 ya Uhuru wa Tanganyika kwa kuwatembelea mwenyekiti wao, Freeman Mbowe na mweka hazina wa baraza la wanawake la chama hicho (Bawacha), Esther Matiko katika gereza la Segerea, imeelezwa kuwa huenda wakaendelea kusota mahabusu kwa muda mrefu.

Mbowe na Matiko walikata rufaa kutokana na kesi ya jinai inayowakabili na wenzao saba, ili isikilizwe na kuamriwa haraka.

Wakizungumza na Mwananchi mwishoni mwa wiki iliyopita katika Mahakama ya Kisutu baada ya kesi ya msingi ya kina Mbowe kutajwa, mawakili wa Serikali Wakuu, Faraja Nchimbi na Dk Zainabu Mango wanaoendesha kesi hiyo walisema bado hawajajua ni lini watawasilisha sababu zao za rufaa.

Walibainisha kuwa kwa sasa bado wanasubiri kumbukumbu za rufaa (mwenendo wa shauri na vielelezo) kutoka Mahakama Kuu. “Bado hatujaandaa sababu za rufaa kwa sababu hatujapata kumbukumbu za rufaa, bado tunasubiri.

Msajili wa Mahakama Kuu atampelekea Msajili wa Mahakama ya Rufani, halafu tutapewa nakala ndipo tutaandaa na kuwasilisha sababu zetu za rufaa ndani ya siku 21, halafu tutasubiri kupangiwa tarehe ya usikilizwaji,” alisema Wakili Nchimbi.

Wakili Mango alisema kusikilizwa haraka au kuchelewa, iko mikononi mwa Serikali, kwa kuwa anayekata rufaa ndiye anayeweza kuifanya rufaa yake ama isikilizwe kwa haraka au ichelewe, kwa kuonyesha au kutokuonyesha uharaka wake.

Utaratibu wa ukataji rufaa

Wataalamu wa sheria wanasema utaratibu wa ukataji rufaa ya Serikali dhidi ya rufaa ya dhamana ya kina Mbowe na Matiko ni moja ya sababu zitakazowafanya waendelee kukaa mahabusu.

Kiutaratibu, rufaa kwa mashauri ya jinai kama linalowakabili Mbowe na Matiko ina hatua kuu mbili.

Kwanza ni kuwasilisha taarifa ya kusudio la kukata rufaa ndani ya siku 10, kwa mdomo au maandishi (Mahakama za Wilaya na za Hakimu Mkazi kwenda Mahakama Kuu); ndani ya siku 14 kwa maandishi (Mahakama Kuu kwenda Mahakama ya Rufani).

Hivyo ili rufaa yoyote ianze kusikilizwa ni lazima upande uliokata rufaa uwe umewasilisha sababu zake za rufaa ndani ya siku 21 (Mahakama ya Rufani) tangu upande unaokata rufaa utakapopata kumbukumbu za rufaa, ndipo inapangiwa tarehe ya usikilizwaji.

Pili, usikilizwaji wa rufaa hauwezi kuanza kabla upande unaokata rufaa kuwasilisha sababu zake za rufaa.

Hivyo, hatima ya rufaa ya dhamana ya kina Mbowe bado imegubikwa na kiza kwa sababu hata rufaa ya Serikali haijulikani itasikilizwa lini na Serikali haijajua ni lini itawasilisha sababu zake za rufaa.

Wawili hao walikata rufaa Mahakama Kuu chini ya hati ya dharura wakipinga kufutiwa dhamana na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kutokana na kesi ya jinai inayowakabili na wenzao saba.

, ili rufaa yao isikilizwe na kuamriwa haraka.

Hata hivyo, usikilizwaji wa rufaa yao hiyo ulikwama baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), kukata rufaa Mahakama ya Rufani, akipinga uamuzi wa Mahakama Kuu kukubali kuisikiliza rufaa hiyo licha ya kuiwekea pingamizi la awali akitaka rufaa hiyo itupiliwe mbali.

Tangu Novemba 23, mwaka huu walipofutiwa dhamana yao na kurejeshwa mahabusu. Ingawa walikata rufaa kwa hati ya dharura ili rufaa yao isikilizwe tofauti na walivyokuwa wakitarajia, lakini kutokana na rufaa ya Serikali kuchelewa kusikilizwa, wataendelea kubaki mahabusu.

Inaelezwa rufaa ya Serikali itachelewa kusikilizwa tofauti na ilivyokuwa kwa rufaa ya kina Mbowe kutokana na sababu mbili, kwanza utaratibu wa usikilizwaji wa rufaa hiyo ya Serikali na pili ni utaratibu wa ukataji rufaa wa Serikali.

Kumbukumbu za rufaa, katika Mahakama ya Rufani, huandaliwa na Msajili wa Mahakama Kuu, akishazikamilisha huzipeleka kwa Msajili wa Mahakama ya Rufani na kisha wadaawa (warufani na warufaniwa) hupewa nakala za nyaraka hizo.

Kisha mrufani atatakiwa ndani ya siku 21 kuwasilisha sababu za rufaa, tangu siku ya kupokea nyaraka hizo (ambayo haijajulikana), na rufaa itapangiwa tarehe ya kusikilizwa.