Mbowe, Matiko watoa salamu za Krismasi, Mwaka Mpya mahakamani

Muktasari:

  • Mwenyekiti wa Chadema,  Freeman Mbowe na mweka hazina wa Baraza la Wanawake la chama hicho (Bawacha), Esther Matiko wataendelea kusota rumande hadi Januari 3, 2019 baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuahirisha kesi yao

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na Mhazini wa Baraza la Wanawake la chama hicho (Bawacha), Esther Matiko jana waliwatakia heri ya Krismasi na Mwaka mpya wafuasi wao wakati wakitoka katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Walitoa salamu hizo kwa wafuasi wao waliokuwa wamekusanyika mahakamani hapo kusikiliza kesi inayowakabili viongozi hao na wenzao sita ambayo iliahirishwa hadi Januari 3, mwakani.

Mbowe na Matiko walifutiwa dhamana na Novemba 23 baada ya kukiuka masharti katika kesi ya uchochezi inayowakabili mahakamani hapo.

Matiko ambaye ni mbunge wa Tarime mjini ndiye alikuwa wa kwanza kuwatakia wafuasi wao heri na kuonyesha ishara ya vidole viwili juu ambayo ni salamu inayotumiwa na Chadema.

“Nawatakia wote heri ya Krismasi na Mwaka mpya, ila mapambano yanaendelea” alisema Matiko baada ya kesi yao kuahirishwa. Baada ya kueleza hayo, Mbowe naye alinyoosha mkono juu na kuwasalimia wafuasi wao, kisha kuwatakia heri ambapo baadhi yao waliitikia na kuwapa pole.

Ndani ya mahakama

Awali, Wakili wa Serikali, Simon Wankyo akisaidiana na Salim Msemo, alidai mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri kuwa kesi hiyo ilikuja kwa ajili ya kutajwa.

Mbowe na wenzake wote walipandishwa kizimbani saa 3:34 asubuhi na kushuka saa 3:38 asubuhi.

Wakili Simon alidai hawana taarifa ya kinachoendelea katika Mahakama Kuu ambako Mbowe na Matiko wamekata rufaa wakipinga kufutiwa dhamana.

Baada ya maelezo hayo waliomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

Hata hivyo, Wakili Faraja Mangula alidai mawakili wa washtakiwa, Peter Kibatala na Sheck Mfinanga wamepata dharura hivyo wanaomba mahakama ipange kesi huyo kutajwa Januari 4.

Akijibu hoja hiyo, Wakili Simon alidai wanaiachia mahakama ipange tarehe itakayoona inafaa. Hakimu Mashauri alisema Januari 4 atakuwa na kazi nyingine, hivyo aliiahirisha hadi Januari 3.

Baada ya kuahirishwa kwa kesi hiyo, Mbowe na Matiko walirudishwa rumande.

Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Mbunge wa Iringa mjini, Peter Msigwa; Naibu Katibu wa Chadema (Bara), John Mnyika; Katibu Mkuu, Dk Vincent Mashinji; Mbunge wa Bunda, Ester Bulaya na Naibu Katibu (Zanzibar), Salum Mwalimu.

Kwa pamoja washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka 13 ikiwemo kula njama, kufanya mkusanyiko wenye ghasia, kuhamasisha hisia za chuki, kushawishi hali ya kutoridhika, uchochezi na kushawishi utendaji wa kosa la jinai kati ya Februari Mosi na 16 jijini Dar es Salaam.

Baadhi ya viongozi waliohudhuria kesi hiyo jana ni Kiongozi wa ACT, Zitto Kabwe; Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Profesa Abdallah Safari na Mjumbe wa Kamati Kuu Chadema, Mwesiga Baregu.