Mbunge awahi dirisha ‘dogo la usajili’ CCM, wanne waapishwa

Muktasari:

  • Mbunge huyo Abdallah Mtolea aliyekuwa jimbo la Temeke ametangaza kujiuzulu na kukihama chama chake cha CUF ikiwa ni siku ya mwisho iliyowekwa na CCM kwa mbunge wa upinzani anayetaka kujiunga na chama hicho.

Dodoma. Wakati wabunge wanne waliojizulu ubunge kupitia Chadema wakiapishwa upya jana kuwa wabunge wa CCM baada ya kupita bila kupingwa, Mbunge wa Temeke (CUF), Abdallah Mtolea amejiuzulu jana ikiwa ni siku ya mwisho iliyotajwa na chama tawala kuwa ya mwisho kwa wabunge na madiwani wanaotaka kuhamia na kupitishwa kuwania tena bila mchakato wa kura za maoni.

Baadaye jana jioni, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole alisema katika taarifa yake kwamba Mtolea ameomba kujiunga na chama hicho akisisitiza kuwa jana ilikuwa siku ya mwisho ya kupokea viongozi wa upinzani.

Taarifa iliyotolewa na Polepole kwa vyombo vya habari imesema Mtolea alitangaza uamuzi wa kuomba kujiunga na chama hicho katika makao makuu ya CCM jijini Dodoma mbele ya Katibu Mkuu, Dk Bashiru Ally.

Mtolea alitangaza kujiuzulu nafasi hiyo akiwa bungeni jana akisema amevutiwa na mageuzi makubwa ya kiuongozi na kazi nzuri inayofanywa na CCM na Serikali yake chini ya Rais John Magufuli na kuvikaribisha vyama vyenye wabunge kufanya mazungumzo naye.

Desemba 8, 2017 akiwa ameambatana na Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa katika mahojiano na kipindi cha Morning Trumpet kinachorushwa na Televisheni ya Azam alizungumzia wimbi la wanasiasa wanaohama vyama vya siasa, Mtolea aliwakosoa wanasiasa hao na kusema wanaisababishia Serikali hasara.

“Hawa wanaosema wamefurahishwa na kazi ya Rais, hivi kumuunga mkono Rais ndio umtie hasara? Kwa sababu ukijivua ubunge, jimbo lile unaliacha wazi na uchaguzi lazima ufanywe kwa matakwa ya sheria, leo kurudia uchaguzi kwa jimbo moja ni takriban Sh70 bilioni, sasa je, unamsaidiaje Rais kwa kuitia hasara,” alisema Mtolea.

Lakini jana bungeni akitangaza kujiuzulu, Mtolea alisema ameamua kujiuzulu nafasi yake hiyo na uanachama wa CUF kuwa ni mgogoro baina ya Profesa Ibrahim Lipumba ambaye ni mwenyekiti wa CUF anayetambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa na Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif.

“Pande hizi mbili tumekuwa tukisigana kiasi ambacho tunahatarisha maisha yetu mpaka mitaani, muda wote mnakuwa katika hofu ya kufukuzwa. Hata mimi hapa kwa taarifa ambazo nimeletewa wakati wowote wiki ijayo ningefukuzwa ndani ya chama,” alisema.

“Nayafanya maamuzi haya bado nikiendelea kutaka kuwatumikia wananchi wa Jimbo la Temeke, ndiyo maana natumia nafasi hii kuvialika vyama vingine ambavyo vina uwakilishi hapa ndani ya Bunge kama kuna chama kinachoona kuwa kinaweza kufanya kazi na mimi basi nakikaribisha tuzungumze tuone kwamba tunaweza kufanya kazi,” alisema.

Akizungumzia uamuzi wa Mtolea, naibu katibu mkuu wa CUF (Bara) ambaye pia ni Mbunge wa Kaliua, Magdalena Sakaya alisema alisema alishapewa onyo mara kadhaa lakini alikuwa hasikii na hivyo yawezekana amejua kuwa anaweza kuchukuliwa hatua za kinidhamu hivyo akaamua kujiwahi.

Muda mfupi kabla ya Mtolea kutangaza uamuzi huo na kuliaga Bunge, wabunge wanne ambao awali walikuwa Chadema kabla ya kujivua uanachama na kuomba tena ridhaa ya kurejea kwenye chombo hicho cha kutunga sheria kupitia CCM ambako walipita bila kupingwa, waliapishwa.

Wabunge hao ni James Millya (Simanjiro), Joseph Mkundi (Ukerewe), Pauline Gekul (Babati Mjini) na Ryoba Marwa (Serengeti).

Awali, akitoa ratiba ya vikao vya Bunge, Ndugai alisema wabunge hao licha ya kupita bila kupingwa, wangeapishwa katika mkutano wa 14 ambao utafanyika Januari mwakani. lakini jana Katibu wa Bunge, Stephen Kagaigai alisema kuapishwa kwa wabunge hao kumetokana na Bunge kupokea majina yao kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Alisema Bunge halina uwezo wa kushughulikia masuala ya uchaguzi, bali hupokea majina kutoka NEC.

“Tume wametuletea majina ya wabunge wateule wanne, sasa tungesubiri nini, kwa hiyo tumetimiza wajibu kwa kufuata sheria,” alisema Kigaigai.